Monday, August 11, 2008

Dr. Rashid ahusishwa na kashfa za Rada


Aliyewahi kuwa Gavana wa benki kubwa Tanzania na mkurugenzi wa Vodacom ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dr. Idris Rashid, amehusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada inayochunguzwa na makachero wa Uingereza.


Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Uchunguzi wa Makosa ya Jinai – Serious Fraud Office (SFO) la Uingereza, Dk. Rashid ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi katika ununuzi wa rada iliyogharimu kiasi cha Sh. 40 bilioni.


Shirika hilo linadai kuwa bei ya rada ilikuwa kubwa kuliko thamani yake na kwamba BAE itakuwa ililipa mawakala kiasi kikubwa cha fedha “kulainisha” baadhi ya viongozi wa serikali ili wakubali bei hiyo.


Dk. Rashid aliteuliwa na Rais Kikwete Novemba 2006 kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO. Mwaka mmoja baadaye, Dk. Rashid aliandika barua ya kujiuzulu lakini rais alimkatalia kujiuzulu.


Uamuzi wa Dk. Rashid kujiuzulu ulitokana na kile alichoita kuamrishwa na Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu, kurudisha umeme aliokuwa ameamua ukatwe, katika kiwanda cha Tanga Cement, jambo ambalo Dk. Rashid alilichukulia kuwa “uingiliaji katika kazi na udhalilishaji.”


Taarifa za kuaminika zinasema Dk. Rashid anamiliki kampuni yenye akaunti nchini Uingereza na kwamba kampuni yake ilimegewa Paundi 600,000 za Uingereza (sawa na Sh. 1.32 bilioni) kutoka akaunti ya kampuni ya Andrew Chenge ambaye tayari anachunguzwa na SFO.


Taarifa za kampuni ya Siemens Plessey System (SPS) zinasema, Dk. Rashid anatajwa kuwa mratibu mkuu wa “taarifa zote kutoka serikalini na BoT.” SPS ndio walihusika kufanya majadiliano ya awali ya ununuzi wa rada hiyo kwa niaba ya Serikali, chini ya ofisa wake aliyetajwa kuwa ni Jonathan Joseph Horne.


No comments: