Tuesday, August 19, 2008

Kikwete apokea riport ya EPA "kisailensa"


RIPOTI ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekamilika, kwa kukabidhiwa kimyakimya kwa Rais Jakaya Kikwete.


Kukabidhiwa kimyakimya kwa ripoti hiyo jana bila kuwepo waandishi wa habari, kunazidi kuweka wingu na kuibua maswali mengi kuhusu mchakato mzima wa uchunguzi huo.


Matokeo ya EPA yamekuwa yakisubiriwa kwa hamu na nchi 11 wafadhili zinazochangia katika Mfuko Mkuu wa Bajeti (GBS), ambazo zimesitisha utoaji wa sehemu ya fedha zake zikitaka hatua zaidi zichukuliwe kwa watuhumiwa kutoka makampuni 22 yaliyoiba kiasi hicho cha zaidi ya Sh 133 bilioni.


Wafadhili, sawa na wananchi walio wengi wanataka kuona hatua zaidi zinachukuliwa kwa wahusika wote wa ufisadi katika EPA.


Kubwa ambalo hadi sasa linasubiriwa, ni kuona na kusikia majina ya wahusika wa ufisadi huo wa mabilioni ambayo yameibwa katika taasisi nyeti ya fedha ya nchi.


Hata hivyo, wakati matumaini yakiwa ni hayo siku ya jana ambayo ilikuwa ni muhimu kwa waandishi kuweza kuhoji na kupata ufafanuzi wa baadhi ya mambo kuhusu mchakato mzima wa uchunguzi huo wa EPA, kiu hiyo haikukidhiwa baada ya timu kukabidhi ripoti kimyakimya.


Kwa mantiki hiyo, kitendo cha waandishi kutokuwepo katika tukio hilo la Rais kukabidhiwa ripoti kuliwanyima fursa wananchi kupata taarifa sahihi ambazo zingetokana na maswali ya waandishi kwa wajumbe wa timu na hata Rais.

No comments: