Monday, August 11, 2008

Tibaigana Anyang'anywa gari na serikali

Serikali imelichukua gari alilolimilki likiwa na utata, Kamanda wa zamani wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana.

SAKATA la mauaji yenye utata ya vijana wawili, wakazi wa Dar es Salaam, Mine Chomba na Hija Shaha Salehe, yaliyotokea mwaka 2006, limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrance Masha, kuagiza magari yote yaliyohusishwa na mauaji hayo, likiwamo analomiliki Kamanda wa zamani wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, kurudishwa ili uchunguzi ufanyike upya.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Waziri Masha, zinaeleza kuwa, magari hayo tayari yamesharejeshwa kwa ajili ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na jinsi yalivyochukuliwa.
Inaelezwa kwamba, magari hayo yanayodaiwa kuwa mali ya marehemu Chomba, yalikamatwa na Polisi kwa muda mrefu, yakidaiwa kuwa ni ya wizi kabla ya kuuzwa kwa njia ya utata.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu juzi, Waziri Masha alisema kuwa, magari hayo yote yamesharudishwa kama alivyoagiza.

"Kama mlisikia wakati wa hotuba ya bajeti yangu bungeni, niliagiza magari yote yarudishwe na tayari yamesharudishwa," alisema Waziri Masha.
Kati ya magari hayo yaliyopaswa kurudishwa ni pamoja na Toyota RAV 4 ambalo lilinunuliwa kwenye mnada wa hadhara na Tibaigana.

Hata hivyo, habari zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa marehemu Mine, zinaeleza kuwa, tayari walishakwenda kumwona Waziri Masha kujua hatima ya suala la ndugu yao.

Mmoja wa ndugu hao, ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema kuwa, walikwenda hivi karibuni kumwoma Waziri Masha na kwamba alisema ameshalishughulikia suala hilo kwa kuagiza magari hayo yarejeshwe.

No comments: