Saturday, August 23, 2008

TUCTA wasitisha mgomo

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limeahirisha mgomo wake wa siku tatu uliopangwa kuanza kesho kutwa na badala yake litasubiri utekelezwaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa juzi bungeni Dodoma.

Kauli hiyo ilitolewa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nestory Ngulla, baada ya kikao cha makatibu wote wa vyama vya wafanyakazi nchini kutafakari kauli ya Rais Kikwete.

Bw. Ngulla alisema vyama vya wafanyakazi nchini na wafanyakazi wote kwa ujumla, wana imani kubwa na Rais Kikwete, kwa kuwa kauli zake zinaaminika na zina uzito wa pekee kama kiongozi wa Taifa na kuzishutumu kauli alizoziita za kejeli, zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bibi Hawa Ghasia.

"Kauli ya Mheshimiwa Rais hatuwezi kuifananisha na kauli za kejeli na zisizoaminika zilizotolewa na Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bibi Ghasia. "Kauli ya Rais aliyoitoa, lazima ipewe uzito wa pekee, tunaamini ahadi aliyoitoa ya kulipa malimbikizo ya mishahara yanayolalamikiwa na wafanyakazi ya Agosti mwaka huu ni ahadi ya kweli," alisema.

Katibu Mkuu huyo, alisema baada ya kuona uzito wa ahadi aliyotoa Rais Kikwete, kikao cha TUCTA kilichokutana jana kilipitisha uamuzi wa dhati wa kuahirisha mgomo huo uliopangwa kufanyika siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 25 hadi 27 mwaka huu, hadi hapo ahadi ya Rais itakaposhindikana kutekelezwa kwa muda alioeleza.

Alisema notisi ya mgomo iliyotolewa awali inaendelea kufanya kazi na itasubiri hadi Septemba 3 mwaka huu, siku ambayo Rais ameahidi kumaliza tatizo hilo na kama hakuna utekelezaji, mgomo utaanza mara moja.

No comments: