RAIS Jakaya Kikwete amewatahadharisha viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) kuwa hawana budi kuwa makini na fedha wanazopata kwa kuwa kutafuna fedha za chama kunaweza kuifanya serikali kuiingilia kati na hivyo kupoteza uhuru wake wa kujiendesha.
Rais Kikwete pia amewataka viongozi wa TFF kutobweteka msaada wa serikali wa kumlipa kocha wa kigeni na badala yake watafute vyanzo vya fedha kwa ajili ya kugharimia jukumu hilo kwa kuwa si la serikali.
Rais Kikwete, ambaye aliahidi kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya michezo nchini, alisema hayo jana wakati akihutubia Bunge la Jamhuri ya Mungano mjini Dodoma jana.
Kikwete alisema TFF isije ikadhani kuwa katika mishahara ya watumishi wa umma, kuna fungu la mshahara wa kocha wa soka.
''TFF wasigeuze ofa yangu kuwa ya milele…suala la kocha si kazi ya serikali. Waanze kujiwekea fungu kwa ajili ya kujijengea uwezo wa kumlipa kocha,'' alisema Kikwete. ''Hizo fedha kidogo wanazopata wasizitafune. Waanze kujiwekea kidogo kidogo; waanze kutengeneza fungu, wasizitafune.
“Pamoja na kwamba kile (TFF) ni chombo cha hiari, wakitafuna fedha watatushawishi tuwaingilie na hivyo watapoteza uhuru wao wa kujiendesha kwa uhuru.”
Kikwete alisema kuwa azma yake na serikali kwa ujumla ni kuona michezo inapiga hatua na hasa soka ndio maana iliamua kutoa msaada wa kiufundi kwa vyama.
Kikwete, ambaye ni shabiki mkubwa wa soka, hakuacha kumwaga sifa kwa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, ambayo alisema sasa imeigeuza nchi kuwa kinyozi baada ya miaka kadhaa ya kuwa kichwa cha mwenda wazimu.
''Nimeleta kocha na nikakubali kumlipa. Hivi sasa Tanzania inafanya vizuri na hivyo si kichwa cha mwendawazimu tena, sasa hivi Tanzania ni kinyozi,'' alisema rais ambaye alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu.
“Nina hakika katika mashindano mengine siku zijazo, kama Cameroon ikipangwa na Tanzania, itaomba ratiba hiyo ibadilishwe. Hata hao Ghana, katika mchezo wa jana (juzi), tumeona mambo yalikuwa magumu kwa Ghana na hadi kipa akaenda kusaidia kufunga.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment