Tuesday, August 19, 2008

Wakatoliki wazuiwa kumpokea Milingo


RAIS wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu, Askofu Thadeus Rwaichi amewataka waumini wa kanisa hilo kutoshiriki katika ujio wa aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Lusaka, Zambia Emmanuel Milingo anayetarajiwa kuzuru nchini hivi karibuni.


Askofu Rwaichi alitoa tahadhari hiyo juzi mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujio wa Askofu Milingo anayetarajiwa kuzuru nchini kati ya Agosti 22 na 25 mwaka huu.


Alisema hatua hiyo inatokana na matukio kadhaa yaliyofanywa na askofu huyo kwenda kinyume na maadili ya kanisa hilo kwa kuamua kuoa .


Askofu Rwaichi, alisema kutokana na kitendo hicho, waumini wa Kanisa Katoliki hawana sababu ya kushiriki katika ujio huo kwani hauna uhusiano wowote na kanisa hilo .


Aidha, alisema hata kama wapo waumini ambao watashiriki kwenye ujio huo watambue wazi kuwa kufanya hivyo ni kinyume na maamuzi ya kanisa hilo. "Naomba kusema kuwa waumini wangu msikengeuke, hata kama wapo watakaoshiriki ujio wa Askofu Milingo lazima wajue wanasimama wapi kwa kuchukua tahadhari kubwa,”alisema Askofu Rwaichi.


Alibainisha kuwa kwa sasa kuna tetesi kwamba Askofu Milingo anaishi nchini Korea baada ya kuasi Kanisa lake kwa kuamua kuoa jambo ambalo ni kinyume na kanisa hilo .

No comments: