Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), limetangaza mgao wa umeme kwa kipindi kisichojulikana. Hatua hiyo imeelezwa kuwa inafuatia kuharibika ghafla kwa mashine tatu za kuzalisha nishati hiyo kwenye kituo cha Songas.
Taarifa fupi iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana jioni na Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, ilieleza kwamba, kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha upungufu wa megawati 110.
Taarifa hiyo iIisema upungufu huo ni sawa na asilimia 16 ya kiwango cha mahitaji ya umeme nchini.
``Shirika limejitahidi kadiri ya uwezo wake kujaza pengo hilo la uzalishaji kwa kutumia mitambo mingine ya gesi asilia na ile ya kutumia maji, lakini bado kutabakia na upungufu wa umeme na kulazimu kufanyika mgao wa umeme wa kiwango cha megawati 40 kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku,`` alisema Badra katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa meneja huyo, mgao ulianza jana jioni sehemu mbalimbali nchini isipokuwa jijini Dar es Salaam.
Aidha, alisema taarifa zaidi kuhusiana na maeneo yatakayohusika na mgao huo zitatolewa leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment