Wednesday, September 24, 2008

Nini Kilimsibu Latoya


MWAKILISHI wa shindano la Big Brother Africa BBA 3 Latoya Lyakurwa amerudi nchini akitokea Afrika Kusini huku akisema yaliyotokea kwenye jumba hilo ni mchezo. 

Latoya aliwasili jana saa nane mchana akiwa na sura ya tabasamu na kuwaomba msamaha Watanzania wote kwa namna moja au nyingine na kuwachosha wakati alipokuwa kwenye shindano hilo. 

“Kutolewa kwangu siyo tatizo kubwa sana kwani kukaa kwenye jumba lile ni sawa na mtu ambaye yuko jela hakuna raha kabisa mle ndani kwani kila mtu anahitaji kuishi maisha ya uhuru kama hivi nilivyo sasa sawa nimeumia lakini nimefurahi kutoka pia” anasema. 

Alilalamikia kitendo cha kutoonyeshwa akiwa anafanya mambo mazuri zaidi ya yale ambayo yalikuwa hayafurahishi. 

Aidha, alisema kuwa alishtuka sana na kupata wakati mgumu pale alipoamriwa na Biggie kuwa anatakiwa kwenda kwenye chumba kichafu ‘Dampo” lakini alilazimika kukubaliana na hali hiyo. 

Latoya alisema kuwa anahisi mshindi wa shindano hilo kwa mwaka huu atatoka Angola ambapo wanawakilishwa na Ricco. 
Latoya ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita anasema malengo yake ya baadaye ni kurudi tena shuleni na kuishi katika maisha yake ya kawaida. 

Wakati huohuo aliyekuwa mshiriki wa BBA2 Tatiana Dos Darego ambaye hivi sasa ni Balozi wa Matende na Mabusha aliwasili jana kwa mwaliko wa Unicef amemtaka Latoya kujituma ili kupata mafanikio. 

Latoya amekuwa mshiriki wa kwanza kutolewa kwenye shindano hilo ambako alidumu kwa takribani majuma manne.

No comments: