Saturday, September 27, 2008

Pinda, Odinga Wazungumiza Serikali za Mseto Afrika


Serikali za Kenya na Tanzania zimesema uundwaji wa serikali za mseto barani Afrika si utaratibu wa kudumu na kuna haja ya kuwapo kwa demokrasia ya kweli, inayotoa haki kwa pande zote zinazoshiriki kwenye uchaguzi. 

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga alisema Dar es Salaam jana kuwa, bara la Afrika lipo katika kipindi cha mpito cha kujiondoa katika mfumo wa udikteta, chama kimoja na tawala za kijeshi. Odinga aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliomshirikisha yeye na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda. 

Alisema, maendeleo ya demokrasia yanatofautiana baina ya nchi na nchi, hivyo wao wanaamini yaliyotokea Kenya na Zimbabwe si mfumo wa kudumu katika siasa za Afrika. “Sisi tulifunga bao lakini refarii akasema eti ni offside, na Grigila naye akasema eti hakujua nani kafunga,” alisema Odinga ili kuonyesha upungufu uliopo kwenye uendeshaji wa uchaguzi Afrika na akadai hata Rais Robert Mugabe alicheza mpira peke yake akasema amefunga bao. 

Waziri Mkuu Pinda alisema ipo haja ya kuwa na mfumo unaotoa haki kwa pande zote na kwamba, wakati mwingine serikali za mseto zinatokana na mazingira ya maeneo husika hasa kuokoa maisha ya wananchi. Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Nishati wa Kenya, Kiraitu Murungi, na Waziri wa Elimu ya Juu wa nchi hiyo, Dk. Sally Kosgei, Waziri Pinda alitoa mfano wa Kenya kwamba, kama upande mmoja ungeendelea kung’ang’ania madaraka, Wakenya wangeendelea kuuana. 

No comments: