Wednesday, September 24, 2008

Tani 34,000 Za Maziwa Zakamatwa


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imekamata na kuzuia zaidi ya tani 34,000 za maziwa ya unga zilizoingizwa nchini hivi karibuni kutoka China.

Kukamatwa kwa maziwa hayo kunafuatia ukaguzi unaoendelea nchini baada ya maziwa yanayotengenezwa China kusababisha vifo vya watoto na kusababisha nchi nyingi duniani kupiga marufuku uagizaji wa maziwa hayo.

Katika msako huo, TFDA imebaini kuwepo mifuko 1629 (sawa na tani 34) ya maziwa ya unga toka China .

Mkurugenzi wa Usalama na Chakula wa TFDA, Raymond Wigege aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa maziwa hayo yalikamatwa mwishoni mwa wiki baada ya kuingizwa nchini siku chache tangu mamlaka hiyo isitishe kutoa vibali vya uagizaji na usambazaji wa maziwa na bidhaa zenye viambata vya maziwa kutoka China.

Alisema maziwa hayo yamezuiliwa kwa mujibu wa sheria wakati uchunguzi zaidi unafanyika ili kubaini kama maziwa hayo yaliyoingizwa yana athari yoyote kwa binadamu au la.

Hivi karibuni TFDA ilitoa taarifa ya kusitisha kutoa vibali vya uagizaji na usambazaji wa maziwa na bidhaa zenye viambata vya maziwa kutoka nchini China baada ya habari kutoka Mamlaka za Udhibiti wa Usalama wa Chakula wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kueleza kuwa bidhaa hizo zina athari kwa binadamu.

Imeelzwa kuwa maziwa hayo au viambata vyake vina sumu aina ya melanmine ambayo huathiri figo kwa watoto.

Hadi kufikia jana watoto zaidi ya watoto 1000 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja waliugua kutokana na kula vyakula hivyo na wanne kati yao wamepoteza maisha.

No comments: