RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Leodegar Tenga ameshindwa kuweka bayana azma yake kama atawania tena nafasi hiyo au la kwenye uchaguzi ujao unaotarajia kufanyika Desemba.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema kuwa ni mapema sana kuzungumzia suala hilo kwa vile bado kuna miezi mitatu kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Alisema yeye analojua ni kwamba uchaguzi upo palepale na utafanyika kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo.
''Niwahakikishie tu kwamba uchaguzi upo pale pale na utafanyika kama katiba yetu inavyojieleza,'' alisema Tenga.
Alisema kuwa endapo atazangumzia suala hilo kwa wakati huu itazusha mijadala miongoni mwa wadau wa mpira hapa nchini na kusahau kujadili mambo muhimu ya kutekeleza programu ya maendeleo.
''Miezi mitatu ni mingi sana siwezi kuweka bayana kama nitaomba nafasi au la kwani kwa kufanya hivyo tutasababisha tuweke pembeni masuala ya maendeleo ya soka na kujadili uchaguzi,'' alisema Tenga.
Tenga alisema kuwa jambo la muhimu ambalo linapaswa kujadiliwa na wadau wa soka hapa nchini ni kufanya tathimini ya ni kipi kimefanyika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake na kupanga mikakati ya siku zijazo.
Aliongeza kuwa TFF ni si mali ya watu wachache bali ni mali ya watu wote hivyo kwa wakati huu sera ya uongozi wake ni kufanya kazi kulingana na utashi wa wadau wa soka ili kupiga hatua ya maendeleo .
No comments:
Post a Comment