MWEZI mmoja baada ya serikali kutangaza uchunguzi wa Jeshi la polisi kuona kama kampuni ya ufuaji umeme ya Richmond (LLC) ilighushi nyaraka kupata zabuni ya kufua umeme wa dharura, tayari baadhi ya watu wenye uhusiano na kampuni hiyo wamehojiwa.
Uchunguzi huo ni sehemu ya hatua za serikali kutekeleza maazimio 23 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Azimio la 17 kati ya hayo 23 linataka mhimili huo wa dola uchunguze kuona kama LLC ilighushi nyaraka kupata zabuni hiyo ya mkataba wa Sh179 bilioni, ambao ulisainiwa Juni 23, 2006 .
Kamishna Manumba alisema polisi inafanya uchunguzi wa kina wa kijinai kwa ajili ya kupeleka kesi mahakamani.
"Uchunguzi wetu ni wa kina," alisema Manumba. "Tunafanya uchunguzi kwa ajili ya kesi, hivyo lazima tupate taarifa za kutosha.
"Hatufanyi uchunguzi wa kisiasa. Uliofanyika awali ulikuwa wa kisiasa tofauti na wa kwetu. Huu ni wa kijinai kwa ajili ya kesi mahakamani."
Alipoulizwa kuhusu baadhi ya watu kuhojiwa, alijibu: "Sasa, huwezi kuzungumzia hadharani uchunguzi unaondelea, kumbuka huu bado ni uchunguzi."
Alipoulizwa kama polisi wake wameenda Marekani kufanya uchunguzi kutokana na LLC kuhusishwa na watu kutoka nchi hiyo, Kamishna Manumba alijibu: "Nafikiri sasa tukisema tutaharibu uchunguzi, elewa tunafanya uchunguzi na unakwenda vizuri."
No comments:
Post a Comment