Wenyeviti hao, John Guninita wa Mkoa wa Dar es Salaam, Clement Mabina (Mwanza), Khamis Mgeja (Shinyanga), Deo Sanga (Iringa) , Onesmo Kangole (Arusha), Hypolitus Matete (Rukwa), Nawab Mulla (Mbeya) na William Kusila (Dodoma), wamechukua hatua hiyo siku chache baada ya serikali kulifungia gazeti hilo kwa miezi mitatu.
Serikali iliamua kufungia gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyoelezea harakati zinazoandaliwa za kumuondoa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kwenye mchakato wa kuwania urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, akiitaja mikoa hiyo kuwemo kwenye mipango hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wenzake katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye jengo la CCM la mkoa jana, Guninita alisema habari hiyo imewasikitisha sana na wanaenda mahakamani kumfungulia kesi mwandishi na kudai fidia.
“Kwa kuwa Kubenea hakututendea haki kwa kutuingiza katika tuhuma nzito ambazo sio za kweli, sisi viongozi nane kama alivyotutaja kwa majina tumeamua kumfikisha mahakamani,” alisema Guninita.
Alisema tayari wameshazungumza na mawakili wao ambao hakuwataja na kwamba muda wowote kuanzia leo Kubenea ataitwa mahakamani.
Alifafanua kuwa kutokana na tafsiri yao kuhusu habari hiyo, wameona kuwa Kubenea anataka kuwagombanisha na mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kuwa wana mpango wa kumng'oa.
Alisema kwamba Kubenea amewapaka matope na kuwafanya wasiaminike kwa viongozi wenzao pamoja na wanachama wenzao wa CCM.
Guninita alieleza kuwa habari iliyochapishwa katika gazeti la MwanaHalisi toleo namba 118 la Oktoba 14 yenye kichwa cha habari ‘Njama za kumng’oa Kikwete zafichuka’ iliyoandikwa na Kubenea ilikiuka maadili ya uandishi.
Alisema lengo la kwenda mahakamani ni kumtaka Kubenea athibitishe ukweli mbele ya sheria juu ya uzushi, uchochezi, na uongo wake mbele ya wananchi ili waweze kuona dhahiri uongo wa madai yake.
“Pia tutadai fidia, kuhusu kiwango... hilo ni suala la kisheria na baada ya kushauriana na mawakili wetu tutajua ni kiasi gani tutadai,” alisema Guninita.
Guninita alikanusha vikali kwa niaba ya viongozi wenzake, kuhusika na taarifa hiyo na kuiita kuwa ni ya kizushi, uchochezi na uongo mtupu.
“Kubenea ameandika habari hizo kwa maslahi yake binafsi na sisi hatuhusiki na taarifa hizo za uongo. Bado ni viongozi watiifu kwa mwenyekiti wetu pamoja na chama chetu kwa ujumla,” alilalamika Guninita.
Akiongea na Mwananchi, Kubenea alisema njia iko wazi kwa wenyeviti hao kama wanataka kwenda mahakamani na kuongeza kuwa hawatapata kitu.
Alisema hizo ni katika harakati za kujikosha kwa mwenyekiti wa taifa wa CCM na kwamba yeye hana wasiwasi wowote juu ya vitisho vyao.
“Kama wanaenda na waende, lakini watashindwa tu, huko ni katika kujikosha na mimi sina wasiwasi,” alisema Kubenea.
No comments:
Post a Comment