Tuesday, October 7, 2008

Lori Laua Watano

WATU watano akiwemo mume na wake zake wawili, wamekufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa baada ya basi dogo walilokuwa wakisafaria kutoka Sirari kwenda mjini Musoma kugongwa na roli la mafuta, ajali ambayo iliwaunganisha kwa muda wagombea ubunge wa vyama vya CCM na Chadema.

Ajali hiyo ilihusisha magari namba T 808 AHU Toyota Hiace mali ya Elizabeth Pebahati, ambalo lilikuwa na abiria 15 na lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KAZ 821 Z lililokuwa na tela namba ZC 7367 ambalo ni mali ya Kampuni ya Primefuels Liquid Transport ya nchini Kenya.

Watu watano waliokuwa wamekaa kiti cha nyuma, akiwemo mwanamume mmoja na wake zake wawili walifariki wakati wengine 10 wamejeruhiwa. Waliokufa walitambuliwa kuwa ni Gati Manyinyi, 60, aliyekuwa na wake zake wawili Msogoro Gati, 55, na Nyanoko Gati, 40, wakati maiti za watu wengine wawili bado hajizatambuliwa.

Majeruhi waliolazwa katika hospitali ya wilaya ni Marwa Mwita (46), Mwita Ndimi (25),Welema Gati (31) ambaye ni mke wa tatu wa Gati Manyinyi.

Wengine waliojeruhiwa ikiwa ni pamoja na mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake ni Victoria Ogeli (32), Orango Ogeli(51), Moyi Marwa Masero(23), Moris Michael (33) pamoja na Dany Nyamongo (29).

Tukio la kuokoa majeruhi na kutoa maiti kwenye gari hilo lilichukua takriban saa mbili na hivyo liliwapa muda wagombea ubunge wa CCM na Chadema kuungana na wananchi wengine kusaidia zoezi hilo.

Wakati fulani wagombea hao, Christopher Kangoye wa CCM na Charles Mwera wa Chadema, walibeba miili ya watu hao kwa pamoja na kuipandisha kwenye gari.

Jasinta Mwikali, ambaye ni mkazi wa Nairobi nchini Kenya, alisema: “Tulipofika eneo hilo dereva alisimama na kuanza kuzungumza na dereva mwenzake wa Hiace nyingine wakiulizana iwapo mbele kuna trafiki, lakini ghafla tuliona roli hilo likija kwa kasi nyuma yetu.

"Mbele pia kulikuwa na roli jingine likija kasi ndipo dereva alipoondoa gari lakini gari letu liligongwa kwa nyuma."

Walisema ilikuwa ni kazi ngumu kuondoa watu waliokuwa kwenye Hiace kutokana na lori hilo kupanda juu yake na ililazimika kutumia lori jingine la mafuta kuivuta Hiace hiyo ambayo ilitoka ikiwa vipande na maiti moja na maiti nyingine kukandamizwa na tairi la roli hilo.

Dereva wa roli hilo ambaye hajajulikana jina lake amekimbia, wakati dereva wa Hiace hiyo, Mwijuma Abasi pamoja na kondakta wake, Robert Daudi walisalimika na walikuwepo katika eneo hilo la ajali wakisaidia uokoaji.

No comments: