Tangazo hilo limetolewa na maafisa wake huku Bw Obama akipiga kampeni katika jimbo la Florida, ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano bega kwa bega na Hilary Clinton, aliyekuwa hasimu wake katika kura za maoni ndani ya chama cha Democratic.
Kampeni ya Bw Obama imeeleza kuwa kuanzia siku ya Alhamisi mgombea huyo ataacha kampeni ikiendelea na kwenda kumtembelea bibi (nyanya) yake, Madelyn Dunham, mwenye umri wa miaka 85.
Ugonjwa
Maafisa wake wamebainisha kuwa ingawa Bw Obama mwenyewe hatakuwepo lakini kampeni zitaendelea kama kawaida, atawakilishwa na watu wanaomwunga mkono akiwemo mkewe Michelle Obama.
Bw Obama ataahirisha shughuli alizokuwa afanye katika mji wa Des Moines jimbo la Iowa na Madison, kwenye jimbo la Wisconsin.
Hali ya bibi yake Bi Dunham, aliyesaidia kwa kiasi kikubwa kumkuza na kumlea Barack, haifahamiki bayana, ingawa mpambe mmoja Bw Robert Gibbs amesema afya yake imekuwa ikidhoofika katika majuma ya karibuni.
Vijembe
Katika mojawapo yake ya hotuba zake aliahidi kupinga hatua za kuwaondoa watu majumbani mwao kwa sababu wameshindwa kulipa mikopo ya kununua nyumba.
Kwa upande mwingine, mgombea wa chama cha Republican, John McCain amekosoa sera za uchumi za hasimu wake akiapa kupeleka nchi katika mweleko mpya.
Akipiga kampeni huko Missouri, jimbo jingine linalogombewa na vyama vyote, John McCain alimshutumu mpinzani wake wa Democratic kwa kuwapotosha wananchi kuhusu mipango yake ya kuongeza kodi.
Kampeni ya Barack Obama imepata nguvu kutokana na Collin Powell aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje katika serikali ya rais Bush kutangaza kumwunga mkono na kumtosa mgombea John McCain wa chama chake cha Republican.
No comments:
Post a Comment