Wednesday, October 15, 2008

Piga!! Mpe Jiwe!! Huyooooo!!!....


Rais wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT, Gratias Mukoba akikwepa mawe kutoka kwa waalimu waliojawa na jazba akikimbilia gari la polisi , mkutano wa maandalizi ya mgomo ulivunjika, Makakama Kuu Divisheni ya Kazi ilizuia mgomo wa walimu.

POLISI jana walilazimika kutumia risasi za moto kutawanya walimu waliokuwa wakiwashambulia viongozi wa chama chao, CWT, waliotaka kuwapa taarifa kuwa mgomo wao umezuiwa na Mahakama Kuu, na badala yake wakasema watatekeleza azma yao ya kugoma kuanzia leo.

"Bora tufe kwa risasi tukaepukana na shida tunazoendelea kuzipata kuliko kuendelea kuishi maisha haya," alisema mwalimu mmoja kwenye mkutano huo ulioanza salama kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, lakini ukavunjika baada ya taarifa hiyo.

"Huu ndio wakati wa kufa tukitafuta haki zetu kwa kuwa tumechoka. Hakuna cha wito tena kwa kuwa hii ni kazi kama nyingine."

"Unajua bwana, hii serikali ina watu wanaotaka kujifanya miungu watu. Sisi tunaanza mgomo kwa aina yoyote ile iwe wa kugoma kuingia darasani au hata kama tutaingia darasani hatutafundisha na kama tukifundisha tutafundisha chini ya kiwango," alisikika mmoja wa walimu hao.

Vurugu, kelele, nyimbo za kulaani, mawe na chupa zilirushwa baada ya rais huyo wa CWT, Gratian Mukoba, kutoa tamko lililoelezea kusitishwa kwa mgomo wa walimu uliokuwa uanze leo nchi nzima kuishinikiza serikali kuwalipa walimu haki zao.

Walimu wanasema kuwa, wanaidai serikali zaidi ya Sh23 bilioni, zikiwa ni malimbikizo ya posho zao mbalimbali, fedha za nauli na pia kudai kupandishwa madaraja na haki nyingine, ambazo serikali imeeleza kuwa zitalipwa na kutekelezwa baada ya kumalizika kwa zoezi la uhakiki wa walimu.


No comments: