Friday, October 3, 2008

Ufaransa Waingilia Suala la EPA

MKATABA wa ukaguzi wa deni la mamilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umekamilika na Kampuni ya Lazard iliyoteuliwa kufanya ukaguzi huo kuanzia mapema mwezi huu.

Uhakiki huo wa Kampuni ya Lazard ya Ufaransa, uunafanyika wakati BoT imepoteza zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo zilizotolewa kwa mafisadi katika mazingira ya kutatanisha.

Taarifa kutoka BoT ambazo zilithibitishwa na Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu, zilisema kuwa mkataba huo uko tayari na Lazard inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote kuanzia sasa.

Profesa Ndulu alisema kukamilika kwa mkataba huo kunatokana na mchakato wa muda mrefu uliohusisha BoT na Benki ya Dunia (WB).

"Ndiyo, tumemaliza kukamilisha mkataba, Lazard inatarajiwa kuanza kazi rasmi mwezi huu," alithibitisha gavana Profesa Ndulu.

Profesa Ndulu alifafanua kwamba, katika mkataba huo Lazard pamoja na mambo mengine itaishauri BoT namna bora ya kuachana na usimamizi wa fedha za EPA.

Akiweka bayana, alisema BoT inataka kubaki katika majukumu yake ya kimsingi na kisheria, ambayo ni pamoja na ile ya Benki Kuu ya mwaka 2006.

Kuhusu muda wa ukaguzi huo, Ndulu alisema mkataba unaeleza kwamba Lazard itapaswa kufanya ukaguzi kwa kipindi cha miezi tisa.

"Jambo kubwa pamoja na mengine ni namna ambavyo wananchi yaani BoT itaachana na majukumu ya usimamizi wa fedha za EPA," aliongeza gavana Profesa Ndulu.

Alisema WB ilishiriki katika kuandaa mkataba huo kwani siku za nyuma, iliwahi kushiriki pamoja na kampuni hiyo kuisaidia BoT katika malipo ya fedha za EPA.

Gavana Ndulu aliongeza kwamba, Lazard ni kampuni ambayo awali ilifanyakazi na BoT katika mambo mbalimbali ikiwemo ushauri wa namna bora ya kuimarisha mfumo wa fedha.

Alisema uamuzi wa kuiteua Lazard unatokana na uzoefu wa kampuni hiyo ya Ufaransa, katika utendajikazi wa BoT hasa katika suala la fedha za EPA.

"Hawa Lizard si wageni ndani ya BoT, siku za nyuma waliwahi kufanyakazi nasi na waliweza kutusaidia,"alisisitiza.

Kuanza kwa ukaguzi huo itakuwa ni hatua moja mbele ya kuondoa mzigo wa usimamizi wa fedha za EPA mikononi mwa BoT.

BoT kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2006, inamajukumu mbalimbali ambayo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za uchumi wa nchi na sekta ya fedha.

Kusitishwa malipo ya EPA kulifanyika mara baada ya kubainika kwa ufisadi huo baada ya ukaguzi ukufanywa na kampuni ya Ernst$Young na matokeo yake kutangazwa na serikali Januari 9, mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, deni la EPA hadi mwaka 1999 lilifikia dola za Marekani 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.

Hata hivyo, kulikuwa na Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na WB, ambao waliokuwa wakidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai.

Katika mpango huo, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza kuwa hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.

Hata hivyo, utaratibu huo ndiyo ulileta matatizo ambayo yalibainika katika Ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka 2005/06, ambao ulifanyika Agosti mwaka 2005, ulionyesha matatizo katika ulipaji wa madeni kwa utaratibu wa idhini ya kulipwa wakala wa mdai katika akaunti ya EPA.

Baada ya hapo, kulitokea hali ya kutoelewana kati ya BoT na Mkaguzi Kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini, aliyegundua tatizo hilo, lakini serikali iliingilia kati na Desemba 4, 2006, ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha ukaguzi huo unafanyika kwa kina ambao ulifanywa na Ernst&Young na kubaini ufisadi wa zaidi ya sh 133 bilioni zililizolipwa kwa makampuni 22.

Kufuatia ufisadi huo, Januri 9 Rais Jakaya Kikwete, alitangazia umma kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, kuhusu kutimuliwa kazi kwa aliyekuwa Gavanawa BoT, marehemu Daud Ballali na kuunda Timu Maalumu chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, kuchunguza, kukamata na kufungua mashitaka dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi huo.

EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo awali ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.

Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT na ndipo mwaka juzi ziliibuliwa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo

No comments: