RAIS Jakaya Kikwete amesema uvumilivu na uhuru unaoonyeshwa na serikali yake katika nyanja mbalimbali nchini, ni mkakati wa kujenga jamii yenye utawala bora.
“Baadhi ya watu wanaiona hali hiyo kama ukosefu wa nidhamu, lakini huu ni mwelekeo wetu wa makusudi ili kujenga uvumilivu na uhuru mpana zaidi na bila shaka tutafika,” Rais Kikwete alimweleza Malkia ll Henrik wa Denmark, jana Ikulu jijini Dar es salaam.
Rais alikuwa anazungumza na malkia huyo aliyko nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku nne baada ya kualikwa na Rais Kikwete.
Ziara hiyo ilianza jana baada ya malkia huyo kupokelewa katika sherehe ya kuvutia kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini.
Rais alimwambia malkia huyo kuwa hatua ya serikali za kujenga uvulivu zinachukuliwa kwa makusudi pamoja na kufahamu kwamba demokrasia nchini Tanzania bado ni changa.
“Tunajua kuwa demokrasia yetu ni changa kabisa, ndio kwanza tumeanza safari ndefu ya kujenga mfumo huo, lakini tunachukua hatua hiyo kw amanufaa ya taifa,” Rais Kikwete alimweleza mgeni wake na kuongeza:
“Tunaishukuru sana Denmark kwa kutuunga mkono katika eneo hilo, kama mnavyofanya katika maeneo mengine hasa ya maendeleo kama miundombinu, jitihada za kupambana na umasikini, virusi vya ukimwi, kufutiwa madeni na utawala bora,” alisema Rais Kikwete.
Rais pia alimshukuru Malkia kwa msaada wa Denmark kwa benki ya CRDB.
“Tunaishukuru Serikali ya Denmark na wananchi wake kwa kusaidia kuunga mkono benki ya CRDB ambayo sasa imekuwa moja ya benki bora zaidi nchini kutokana na msaada wenu,” alisema.
Rais Kikwete alimwweleza Malkia huyo kwamba kwa kiasi fulani, ziara hiyo imemkamilishia historia.
''Januari 10, mwaka 1970, nilimpokea baba yako, Mfalme Frederick wa Tisa wakati alipokuja kufungua Kituo cha Elimu cha Kibaha, kilichogharimiwa na nchi za Nordic.''
''Wakati huo nilikuwa mwanafunzi pale Kibaha Sekondari na nilijipanga mstari wa mbele kumshangilia Mfalme alipowasili. Ni jambo la ukumbusho kwamba leo nakupokea wewe mtoto wa Mfalme Frederick, ukiwa tayari Malkia. Kwa hakika mzunguko wa historia umekamilika.''
Rais Kikwete pia ameishukuru Serikali ya Denmark kwa kumteua (yeye) kuwamo katika Tume ya Ajira kwa Afrika iliyoteuliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
1 comment:
Twende mbele turudi JK JK unastahili pongezi kubwa mnooooooooooo.... Nakuaminia JK ni mtu wa Familia
Post a Comment