Mamlaka wa Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imesema baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa za petroli wameteremsha bei licha ya kuwa wako baadhi ambao hawajafanya hivyo kwa visingizio kadhaa.
Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu alisema jana kuwa wafanyabiashara ambao hawajapunguza bei hizo ni wale ambao bado wanabishana na Ewura juu ya fomula inayotumika kuuzia mafuta na wengine wanatoa visingizio vya kuwa na akiba ya mafuta waliyoagiza siku za nyuma kabla ya bei kushuka.
Alisema baada ya barua ile iliyoandikwa na Ewura kwenda kwa wafanyabiashara, wengine walionyesha wasiwasi wa kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani ambayo kwa dola moja ni Sh 1,300. “Lakini wengi wameshusha bei na ninyi ni mashuhuda… katika baadhi ya vituo, bei zimeshuka hadi shilingi 1,500 kwa petroli, dizeli inauzwa shilingi 1,575 na mafuta ya taa 1,290,” alisema Masebu.
Alivitaja baadhi ya vituo kama vya BigBon, Total, Mt. Meru na Gapco kuwa vimeteremsha bei. Lakini hata hivyo, alikiri kuwa vituo kama vya BP havijateremsha bei kwa kisingizio cha kuwa na akiba ya mafuta ya nyuma.
Alisema licha ya bei ya mafuta kushuka katika soko la dunia, lakini bei za usafirishaji, bima (CIF) na gharama za bandari, ziko palepale hali inayowalazimu wenye vituo vya mafuta kuendelea kuuza kwa bei kulingana na gharama hizo.
Alisema wakati wamewaandikia barua wafanyabiashara, baadhi waliahidi kuteremsha, lakini wakaomba kufanyike fomula mpya ya kupata vigezo vya bei ya mafuta, wengine wakasingizia kushuka kwa thamani ya shilingi pamoja na kodi mbalimbali zinazotozwa nchini.
Alisema Ewura inatambua kuwapo kwa mafuta yaliyoagizwa siku za nyuma, lakini akaonya kuwa Ewura haitasita kuchukua hatua iwapo wafanyabiashara hao wataendelea kudanganya kwa kisingizio hicho. “Mamlaka yetu inafuata sheria katika kutekeleza udhibiti, hakuna mfanyabiashara aliye juu ya sheria, wale ambao wataendelea kukaidi kushusha tutaangalia sheria inavyosema,” alisema Mkurugenzi huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment