HATIMAYE mafisadi wanaotuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jana walifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka ya kughushi na kujipatia mamilioni ya fedha toka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jumla ya watu 10, akiwemo mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel, pamoja na wafanyakazi wa BoT walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi hiyo ya aina yake ilishuhudiwa na wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ilichukua zaidi ya saa tano na kumalizika saa 11:45 jioni wakati muda wa kazi unaisha saa 10.30 jioni.
Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa nyakati tofauti huku mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo, Johnson Lukaza akipandishwa peke yake kujibu tuhuma za kula njama na kughushi na kuiibia BoT zaidi ya Sh6.3 bilioni.
Mbele ya Hakimu, Euphemia Mingi, wakili wa serikali Winie Koroso alidai kuwa, kati ya Desemba 2003 na 2005 mshitakiwa alighushi hati ya kuhamishia mali toka kampuni ya Kernel na Maruben ya nchini Japan ambayo ilikuwa inaonyesha imetolewa Februari 4 mwaka 2005.
Koroso alidai kuwa baada ya kughushi hati hiyo aliiwasilisha BoT jijini Dar es Salaam na kujipatia kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mingi aliahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 18 itakapotoa maamuzi ya dhamana.
Katika kesi nyingine washitakiwa watatu akiwemo Jeetu Patel na ndugu zake wawili Devendra Patel na Amit Nandy walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama na kuiibia BoT zaidi ya Sh 2.5 bilioni.
Washitakiwa hao, ambao walifikishwa mbele ya Hakimu Neema Chusi, kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 7 na Desemba 7 mwaka 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia BoT Sh2,599,944,456.12 na kuziwakilisha katika kampuni ya Matsushita Electric Trading.
Katika kesi hiyo mshitakiwa wa tatu Amit Nandi anadaiwa kughushi hati iliyoonyesha kuwa kampuni hiyo ya Matsushita inaidai BoT kiasi hicho cha fedha.
Wakili Koroso aliendelea kudai kuwa Septemba 2 mwaka 2005 washitakiwa walikula njama ya kuiibia BoT Sh3.9 bilioni baada ya kusaini mkataba kati ya kampuni ya Bina na C. Itoh za nchini Japan.
Washitakiwa hao walikana mashtaka yao na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi leo itakapotoa maamuzi ya dhamana.
Mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia pia alipandishwa kizambani tena na ndugu zake watatu, wakiwemo wawili wa awali na Ketan Chohan aliyeongezeka wakikabiliwa na tuhuma za kughushi mkataba wa Kampuni ya Bina Resort na Itoh wakituhumiwa kula njama na kuibia BoT zaidi ya Sh3.9 bilioni.
Pia wafanyakazi watano wa BoT, akiwemo mtu na mke wake, walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama ya kuiibia benki hiyo.
Washitakiwa hao ni pamoja na Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Devis Kamungu, Godfrey Moshi na Iddah Mwakale, ambao kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 23 mwaka 2003 na Oktoba 26 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia BoT.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kugushi mkataba wa makubaliano wa kampuni ya Changanyikeni kwa kutumia saini ya meneja wa kampuni hiyo, Samson Mapunda na kujipatia Sh 8.5 bilioni mali ya BoT, lakini walikana mashitaka yao na kurudishwa tena rumande hadi leo mahakama itakapotoa maamuzi ya dhamana.
Hata hivyo ni makampuni machache kati ya makapuni yaliyohusika katika wizi huo ambayo jana yalitajwa kuhusika na wizi huo.
Kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao kunatokana na ya mafisadi hao walioshindwa kurejesha sh 64 bilioni kati ya sh 133 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo.
Macho ya wengi yalikuwa kwa mtuhumiwa Jeetu Patel, ambaye alionekana kuwa kigogo pekee kati ya wafanyabiashara kumi waliofikishwa mahakamani jana.
Kilichovutia zaidi ni namna Jeetu alivyokamatwa. Kukamatwa kwake kunaonekana kulipangwa kisayansi kwa kutumia mbinu mahiri za kikachero ambazo zilipangwa na Kurugenzi ya Upelelezi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi iliyo chini ya Robert Manumba na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP).
Taarifa ambazo zilipatikana jijini Dar e s Salaam jana zinasema kukamatwa kwa Jeetu kulifanywa kwa siri kubwa, kiasi cha mfanyabiashara huyo kutohisi lolote.
Duru hizo za kiserikali zililidokeza gazeti hili kwamba, jana, mnamo saa 4:00, asubuhi Jeetu alipigiwa simu akaelezwa kwamba anahitajika kwa DPP, Eliazer Feleshi ambaye alikuwa pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.
Wakati Jeetu akiwa anasita, alipigiwa tena simu akisisitiziwa kuhitajika kwa DPP na DCI ambao walikuwa wakimsubiri kwa ajili ya mazungumzo.
"Alipigiwa simu asubuhi, akaelezwa kuwa anapaswa kuja kwa DPP na DCI wako wanamsubiri. Mara ya kwanza akawa ana sitasita kuja; akapigiwa tena kuelezwa kwamba DCI na DPP walikuwa wakimsubiri hivyo anapaswa kwenda," zilisema duru hizo za kiserikali na kuongeza:
"Hakuwa akijua kabisa kwamba atapandishwa mahakamani. Alivyofika tu akaelezwa anapaswa kwenda mahakamani kusomewa mashitaka, hivyo ndivyo jinsi alivyokamatwa Jeetu."
Jeetu na makampuni yake tisa anatuhumiwa kujipatia Sh10.3 bilioni kwa madai ya kutumia nyaraka na kumbukumbu za kughushi, kitu ambacho ni kosa la jinai.
Duru nyingine zilisema mbali ya Jeetu, hata mtuhumiwa Johnson Rwekaza hakuwa akijua bali alipigiwa simu asubuhi na kuelezwa anapaswa kupanda kizimbani.
Duru hizo ziliongeza kwamba, watu wengine watano wa kampuni ya Changanyikeni Residential Complex, walijisalimisha wenyewe polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
"Hawa wa Changanyikeni Complex walijisalimisha wenyewe baada ya kupata taarifa kwamba, wanahitajika kwa ajili ya kufika mahakamani kusomewa mashitaka," ziliongeza duru hizo.
Watuhumiwa hao na wengine kumi jana walipelekwa rumande na msafara wa magari manne ambao uliondoka Mahakama ya Kisutu mnamo saa 12:30 jioni huku ukiwa na askari wenye silaha katika magari mawili aina ya Land Rover, Defender.
Msafara huo uliongozwa na makechero waandamizi ambao walikuwa wametanda katika Mahakama ya Kisutu saa mbili kabla ya watuhumiwa kufikishwa mnamo saa 7:00 mchana.
Kufikishwa mahakamani kwa akina Jeetu ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye alionya kwamba, wafanyabiashara ambao wangeshindwa kurejesha fedha ifikapo Oktoba 31, walipaswa kufikishwa kizimbani ifikapo Novemba mosi.
No comments:
Post a Comment