HADI mwaka 2010, kampuni ya kigeni ya Saskatel inayosimamia uendeshaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) itakuwa imejichotea Sh. 38 bilioni, imefahamika.
Saskatel ni kampuni ya Canada iliyoingia mkataba wa miaka mitatu na serikali ya Tanzania katikati ya mwaka jana, ikiwa ni miaka miwili baada ya TTCL kuzamishwa kutokana na mkataba wa kwanza uliowaingiza MSI/Detecon na kutekelezwa “kishkaji.”
Taarifa za ndani ya TTCL na serikalini zimesema mkataba mpya una matatizo mengi yanayozidisha utafunaji wa fedha za kampuni hiyo iliyokuwa na mtandao madhubuti wa simu za mezani ambao ulienea nchi nzima.
TTCL iliyokuwa na mali zisizohamishika za thamani ya zaidi ya Sh. 500 bilioni, sasa imebaki kama mjane aliyenyang’anywa mali ya urithi.
Majengo, mitambo na viwanja ambavyo vilikuwa mali ya TTCL vilinyofolewa kwenye kampuni. Hazina kubwa ya wataalamu katika kada mbalimbali za ufundi katika Chuo cha Posta cha Kijitonyama, Dar es Salaam nayo ilibomolewa, chuo kusambaratika na mitambo yake kung’olewa.
Vyanzo vya habari vimebainisha kuwa moja ya matatizo katika mkataba wa Saskatel na serikali ni kuhusu gharama za kutunza maofisa wa Saskatel na familia zao.
Jumla ya maofisa 12 wazungu ambao waliletwa nchini kwa madai kuwa ni wataalam wa Saskatel, wanalipwa na kuhudumiwa na TTCL kwa muda wote wa mkataba badala ya kugharimiwa na Saskatel.
“Saskatel wana mkataba. Kama wanaleta wataalam, basi ni wao wanaostahili kuwalipa na siyo TTCL. Gharama za kuwaleta nchini, kuwatunza wao na familia zao na hata gharama za likizo zao, vyote vinategemea TTCL. Kwa nini?” Anauliza ofisa mmoja mwandamizi wa shirika hilo.
Kadhalika, wakuu wa idara na vitengo ambao ni Watanzania, walioajiriwa kwa mkataba na Saskatel, nao wanalipwa mishahara kwa fedha zinazozalishwa na TTCL.
Hata pale kazi za Saskatel zinapokwama kwa sababu ya majanga ya kimaumbile – kwa mfano mafuriko na tetemeko la ardhi yatakayosababisha kuharibu mtandao wa mawasiliano – gharama za kurudisha mtandao, zinapaswa kulipwa na TTCL, unaeleza mkataba.
Tatizo jingine ni kipengele kinachotaka Saskatel walipwe kila baada ya mwaka mmoja “malipo ya ada ya mafanikio” lakini haielezwi ni vigezo gani vitatumika kupima mafanikio hayo na utaratibu upi wa kupanga malipo yake.
Kwa hali yoyote ile, hii ni njia ya kuchuma kwenye “shamba la bibi” kama walivyofanya MSI/Detecon na kujenga himaya ya Celtel ya kimataifa.
Kampuni ya Celtel ilichipuka katika MSI/Detecon; ikitumia mitambo ya mawasiliano ya TTCL na kujitanua hadi nchi za Uganda na Kenya kabla ya kusambaa nchi nyingine jirani.
Kwa kutumia kiini kilekile cha Tanzania, Celtel ilijibadilisha na kuwa Celtel International na baadaye kujitanua na kuwa mwanachama wa kundi la makampuni ya MTC (Mobile Telecommunication Company) ya Ghuba.
Hivi karibuni, Celtel International imejibadilisha na kuwa ZAIN. Yawezekana Saskatel inajiwekea msingi kutoka shamba lilelile la “bibi” ambako mikataba imekuwa haizingatii maslahi ya raslimali za Watanzania.
“Sikiliza ndugu yangu; wanaoingia mikataba hii wanajua wanachofanya. Wanawekeza hukohuko. Hatuwezi kulaumu watu wa nje peke yao maana hii hujuma inaanzia hapa kwetu,” ameeleza ofisa huyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia MwanaHALISI, tayari Saskatel imepeleka ripoti kwao kuelezea “utekelezaji wa mkataba,” kitendo kinachoashiria kuanza hatua za kudai na kuchota malipo ya kwanza.
Kwa mujibu wa mkataba, Serikali ya Canada ndio mdhamini wa mkataba kwa Saskatel, na utaratibu unaelekeza serikali ndizo zitawajibika kuwasiliana kuhusu malipo hayo.
Lakini kumezuka utata hapo, kwa kuwa waliyoyaeleza hayakuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL inayoongozwa na Profesa Mathew Luhanga.
Kwa sababu hiyo, inasemekana Profesa Luhanga amelalamika na kuna mvutano kati ya Bodi na wakuu wa Saskatel.
Taarifa zaidi zimesema Saskatel wamejipendelea kwa kuwa hata kwa yale maeneo yasiyoleta tija yoyote kwa TTCL, wametaja kama yamefanikiwa.
Wakati miradi karibu yote ya maendeleo iliyopangwa na TTCL katika mpango wake wa maendeleo tangu mwaka 2006 imekwama baada ya kupuuzwa na wawekezaji, Saskatel wamesema wameitekeleza vema.
Baadhi ya maeneo wanayodai yamepiga hatua kutokana na utaalamu waliotoa, ni kuongeza laini 7,347 za simu za kulipia kabla na laini 7,122 za kulipia baada ya kutumia.
Ripoti ya Saskatel imebainisha mafanikio katika mtambo wa kuandaa bili za wateja (CCBS) wakati mtambo huo haufanyi kazi.
Mafanikio mengine yanayotajwa ni ufanisi katika kutengeneza simu ndani ya saa 24 baada ya wateja kuripoti hitilafu.Eneo jingine ambako Saskatel haikusema ukweli, ni kuhusu maslahi ya wafanyakazi wa TTCL. Hadi sasa hakuna maafikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi juu ya muundo wa mishahara.
Kinachoonekana ni juhudi za menejimenti kuwagawa wafanyakazi kwa misingi ya mishahara na marupurupu; hatua ambayo imesababisha wasiwe na umoja katika kudai haki zao.
Kwa mfano, viwango vya mishahara vilivyowekwa, vinatofautiana sana kutoka tabaka la juu la mameneja hadi la chini.
Saskatel waliingia TTCL baada ya kujengewa mazingira na wawekezaji wa awali – MSI/Detecon – ambao wakati wanaondoka, walipendekeza TTCL iendeshwe na kampuni inayojitegemea. Saskatel ilikuwa kampuni ya ununuzi wa zana zilizotumiwa na MSI/Detecon.
Kulingana na vyanzo mbalimbali vya taarifa, wakati Saskatel wanaingia TTCL, hesabu zilizoishia 31 Desemba 2006 zilikuwa zinaonyesha kampuni iliingiza mapato ya Sh. 92.018 bilioni na mapato kabla ya kodi na riba yalikuwa Sh. 16.210 bilioni.
Kwa mujibu wa waraka uliosomwa kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu mwaka jana, TTCL ilikusudia kuimarisha huduma za simu na kupanua mtandao wa mawasiliano nchi nzima kwa kutumia bajeti ya Sh. 212 bilioni.
Miongoni mwa miradi hiyo ni kusambaza simu za mkononi zisizotumia waya (CDMA). Simu hizo zilizotakiwa kuenea kwenye miji mikuu ya mikoa na wilaya kote Bara na Zanzibar ifikapo Juni 2007.
Kuingia kwa Saskatel hakujaleta nafuu. Mradi huo haujatekelezwa hata ndani ya Dar es Salaam kwenyewe ambako mtandao wake ni duni mno.
MwanaHALISI lina taarifa kuwa mali za TTCL zisizohamishika zimefisidiwa kiasi kwamba baadhi ya nyumba zake ziliuzwa kwa bei ya kutupa kupitia iliyokuwa kampuni ya Simu 2000 Ltd.
Kwa mfano, imeelezwa kuwa nyumba aliyokuwa akitumia Mkurugenzi Mkuu wa TTCL iliyoko mtaa wa Chake Chake eneo la Masaki Dar es Salaam, iliuzwa kwa kiasi cha Sh. 20 milioni wakati thamani yake ilikaribia Sh. 500 milioni.
Nyumba hiyo, kwenye kiwanja Na. 308 aliuziwa Marten Lumbanga, Balozi wa Tanzania nchini Uswisi ambaye wakati wa mchakato wa kubinafsisha TTCL ikiwemo uuzaji wa mali zake kupitia Simu 2000 Ltd, alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Nyumba nyingine za TTCL zilizouzwa kwa “bei poa” zipo Kurasini, Chang’ombe, Upanga, Ilala na Oyster Bay. Nyingine zipo kwenye makao makuu ya wilaya nchini kote ambako pia kuna viwanja vyake.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Maua Daftari aliliambia Bunge kuwa serikali imepata Sh. 18.327 bilioni kutokana na uuzaji mali za TTCL uliofanywa na iliyokuwa kampuni ya Simu 2000 Ltd.
Waziri hakusema ni mali zipi ziliuzwa, ingawa mali zilizothibitishwa kuwa ni za TTCL alisema ni majengo 103 na viwanja 30.
Alikuwa akijibu swali la Victor Mwambalaswa (Lupa, CCM) aliyetaka kujua mali za TTCL zilizohodhiwa na Simu 2000 Ltd na kiasi gani kilipatikana baada ya kuuzwa.
No comments:
Post a Comment