UWEZEKANO wa kutokea vurugu kwenye ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), jana ulipotea baada ya polisi kuweka ulinzi mkali, huku chombo hicho kikiweka wana usalama binafsi, maarufu kama 'mabaunsa' kukabiliana na kikundi cha vijana wa Kiislamu waliodaiwa kukusudia kuvamia ofisi hizo kwa lengo la kupindua utawala.
Wakati mikakati hiyo ikiripotiwa kufanywa, viongozi wote wa Bakwata hawakuwepo jijini Dar es Salaam na kwamba walikuwa mjini Dodoma kwa ajili ya mkutano mkuu unaotarajiwa kuanza leo kujadili marekebisho ya katiba ya baraza hilo.
Kwenye ofisi za Bakwata jana maajira ya saa 6: 10 mchana, gari la kwanza la polisi aina ya Land Rover lenye namba PT 0751 liliwasili katika eneo hilo likiwa na askari wenye silaha, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni na kuegeshwa kando kidogo ya lango kuu la kuingilia kwenye ofisi hizo na dakika 30 baadaye liliingia gari jingine la polisi likiwa na askari.
Askari hao walionekana kurandaranda katika maeneo hayo huku wengine wakionekana kuwa tayari kwa lolote ambalo lingeweza kutokea katika eneo hilo.
Mbali na ulinzi huo, pia kulikuwapo vijana maarufu kwa jina la 'mabaunsa' walioandaliwa na utawala wa Baraza Kuu kwa ajili ya kudhibiti hali ya amani iliyokuwa tete katika eneo hilo.
Vijana hao wenye vifua vipana walikuwa katika kila kona ya Msikiti wa Alfarook, huku vikundi vidogo vidogo vya watu vikibadilishana mawazo juu ya kadhia hiyo.
No comments:
Post a Comment