Saturday, September 20, 2008

Waswazi Kuchagua Wabunge


Nchi ya Swaziland kwa mara ya kwanza inapiga kura kuchagua wabunge chini ya katiba mpya, huku chagizo zikiongezeka za wanaharakati wanaodai demokrasia zaidi.

Vyama vya siasa vimepigwa marufuku katika nchi hiyo ndogo ya Afrika yenye utawala wa Kifalme.

Serikali imesema inatarajia watu wengi watajitokeza kupiga kura, katika uchaguzi utakaoshuhudiwa kwa mara ya kwanza na waangalizi kutoka nje.

Baadhi ya raia wa Swaziland wamekuwa wakimlaumu Mfalme wao Mswati III kwa kuiingiza nchi hiyo katika lindi la umasikini na pia kwa kushindwa kukabiliana na maradhi ya Ukimwi.

Mfalme huyo amekuwa madarakani tangu mwaka 1986. Hivi karibuni serikali yake ilifanya karamu ya kifahari iliyogharimu dola milioni 12 kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa mfalme na pia miaka 40 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka Uingereza.

Askari polisi wanalinda vituo vya kupigia kura nchini kote, baada ya kutokea jaribio la maandamani kutoka kwa wanaharakati.

Jana viongozi kadha wa wanaharakati hao walikamatwa baada ya kujaribu kufunga mpaka na Afrika KUsini, katika hatua waliyosema ilikuwa na lengo la kuelezea matatizo yanayoikabili nchi hiyo.

No comments: