Wednesday, October 15, 2008


Msemaji wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, amesema Bwana Thabo Mbeki ana matumaini makubwa ya kuokoa mazungumzo yaliyokwama ya kugawana madaraka nchini Zimbabwe.

Msemaji huyo amesema wana hakika watafanikiwa kumaliza suala hilo, bila kujali muda utakaotumika kulitatua.

Mazungumzo ya kugawana madaraka yalikwama baada ya Rais Robert Mugabe mwishoni mwa wiki kuwateua katika wizara nyeti mawaziri kutoka chama chake cha Zanu-PF.

Leo hii Bwana Mbeki alifanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Zimbabwe kabla Bunge halijakutana kwa mara ya kwanza tangu wabunge walipoapishwa.

Bunge lenye wabunge wengi kutoka chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC)linatazamiwa kujadiliana suala la kuifanyia marekebisho katiba, ili kumuwezesha kiongozi wa upinzani Bwana Morgan Tsvangirai awe Waziri Mkuu ikiwa ni moja ya masharti muhimu chini ya makubaliano.

Hata hivyo Bwana Tsvangirai ametishia kujiondoa katika mazungumzo hayo baada ya serikali kutangaza wizara muhimu siku ya Jumamosi ikiwemo ziara ya ulinzi, mambo ya ndani, mambo ya nje na sheria kwa chama cha Zanu-PF.

Bwana Tsvangirai anataka nafasi zote za mawaziri zipitiwe upya katika mazungumzo na Bwana Mbeki aliyesimamia mapatano hayo mwezi uliopita, lakini chama cha Zanu-PF kimesema nafasi moja tu ya wizara ya fedha ndio inaweza kujadiliwa.

No comments: