Wednesday, October 15, 2008

Ripoti Yasubiriwa Kenya Juu ya Ukabila


Viongozi wa serikali ya umoja nchini Kenya watapokea ripoti iliyochunguza ghasia za kikabila mapema mwaka huu baada ya matokeo ya uchaguzi kupingwa.

Tume iliyopewa kazi hiyo ilitakiwa kuchunguza namna vyama vya siasa pamoja na vikosi vya usalama vilivyojihusisha katika ghasia hizo.

Mwandishi wa BBC nchini Kenya Peter Greste amesema mgawanyiko uliotokea baada ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana umekuwa wa kikabila na Kenya ilikuwa ikielekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Zaidi ya watu 1,500 waliuawa na wengine wanaofikia 300,000 walilazimika kuzihama nyumba zao.

Baada ya usuluhishi wa kimataifa, Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga walitiliana saini makubaliano ya kugawana madaraka mwezi wa Februari na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Bwana Odinga akawa Waziri Mkuu.

Jaji Philip Waki aliongoza tume ya uchunguzi iliyoteuliwa kufuatia mapendekezo ya jopo la wasuluhishi la Umoja wa Mataifa walioongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Jopo hilo liliwasilisha ripoti yao kwa Bwana Kibaki na Bwana Odinga.

Siku ya Jumanne baraza la mawaziri la Kenya lilisema litatekeleza mapendekezo ya tume nyingine iliyochunguza wizi wa kura uliojitokeza, tume iliyotoa mapendekezo ya kubadilishwa Tume ya uchaguzi.

No comments: