Sakata la madai ya walimu na ufungwaji wa vyuo vikuu nchini, limezidi kuzua mambo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuandaa maandamano ya amani.
Maandamano hayo yamepangwa kufanyika keshokutwa, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwasilisha tamko lao Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuhusiana na kadhia hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa CUF iliyotumwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Mbaralah Maharagande, kupitia mtandao wa kompyuta jana, maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia katika majengo ya Karimjee saa 8:00 mchana na kwenda moja kwa moja hadi wizarani hapo.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe, amepelekewa na chama hicho barua yenye Kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/KR/MMU/IF/2008/43 ya Novemba 18, mwaka huu, ikimtaka apokee maandamano hayo.
Nakala ya barua hiyo, imepelekwa pia, kwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Sehemu ya Mlimani, Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Chang`ombe (DUCE) na kwa vyombo vya habari.
CUF pia, imemwandikia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala barua rasmi, Marais wa CWT, Wanafunzi DUCE na UDSM kuwaarifu kuhusu maandamano hayo.
Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini, juzi walianza mgomo kushinikiza serikali iwalipe madai yao kabla ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, kuzuia kwa mara nyingine juzi mgomo huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment