Thursday, November 20, 2008

Tanesco na Dowans

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imeshtukia mchezo mchafu uliosukwa na Bodi iliyopita ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wa kupitisha uamuzi wa ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Dowans. 

Kulingana na chanzo chetu cha habari, Bodi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Balozi Fulgence Kazaura, Iliridhia Tanesco kununua mitambo ya Dowans. 

Chanzo hicho kilisema hatua hiyo ilifikiwa na bodi kwa kigezo kimoja cha kwamba, mitambo hiyo ni mipya ilhali imefanyakazi kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kuingizwa nchini. 

Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika wiki ya mwisho wa mkutano wa Bunge wa 13 mjini Dodoma, ilimwita Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na kumuonya dhidi ya uamuzi huo. 

``Tulimuonya kuwa kuchukua uamuzi huo ni ukiukaji na dharau dhidi ya agizo la Bunge...ni mwendelezo wa maslahi binafsi ya watendaji waandamizi wa Tanesco kwenye Dowans, kilisema chanzo chetu na kuongeza: 

``Hata Kamati Teule ya Bunge ya Kuchunguza Mchakato wa Ushindi wa Zabuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura iliyotolewa kwa Richmond, iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilibainisha haya. 

Katika taarifa ya Kamati ya Mwakyembe, inaonyesha kuna baadhi ya watendaji waandamizi wa Tanesco walishinikiza ushindi wa zabuni hiyo na baadaye kuacha kazi na kujiunga na Kampuni ya Richmond Development na sasa Dowans. 

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati na Waziri Ngeleja zinaeleza kuwa, mbunge mmoja (jina tunalo), alifikia hatua ya kumweleza iwapo uamuzi huo utachukuliwa itakuwa imethibitisha hisia zilizoko mitaani kuwa mtandao wa kampuni moja (jina tunalo) kuchota fedha za serikali unakamilika. 

``Hatua hiyo itathibitisha hisia zilizoko mitaani kuwa mtandao wa kuchota fedha za serikali unakamilika,``chanzo chetu kilimkariri mbunge huyo. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shelukindo, alithibitisha kumwita Ngeleja na kwamba, kilichosalia ni kusikiliza uamuzi utakaochukuliwa na serikali. 

Tayari, Kampuni ya Dowans Holding imetangaza zabuni ya kuuza mitambo hiyo, ambayo katika hitilafu iliyotokea hivi karibuni kwenye mitambo ya Songasi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, alisema kama hali ingeendelea kuwa mbaya walikuwa wakipanga hata kununua mitambo hiyo. 

Kashfa ya Richmond sasa Dowans, ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kulazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao. 

Hata hivyo, miongoni mwa baadhi ya mapendekezo ambayo hayajatekelezwa ni kumuwajibisha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko. 

Jitihada za kumpata Waziri Ngeleja na Dk Rashid kutoa ufafanuzi wa suala hilo hazikufanikiwa kwani simu zao zilikuwa hazipatikani zikiashiria ama zimezimwa au ziko nje ya mtandao.

No comments: