Saturday, November 1, 2008

Juhudi Mpya za kuzima Mzozo wa Congo


Kumbukumbu za mauwaji ya Rwanda yaliyomalizika kwa vifo vya takriban watu milioni moja zimeinua hisia za jumuia ya Kimataifa.

Umoja wa Afrika umeshutumu hatua ya waasi wa Laurent Nkunda na kutaka kurejelewa kwa mazungumzo ya amani.

Mawaziri wa mashauri ya nje wa Uingereza na Ufaransa wanazuru sehemu hio ya Dunia kukutana na Ma Rais Kagame wa Rwanda na Rais Joseph Kabila wa Congo.

Lengo la Mawaziri hao ni kuwashawishi viongozi hao juu ya tamaa ya kutumia ushawishi wao kuzima mzozo huo.

Ingawaje Ufaransa imetowa pendekezo la kutuma vikosi vya kuhifadhi amani vikiongozwa na jeshi la Ulaya, hakuna dalili za kuonyesha kua kuna hamu yoyote ya Kimataifa ya kutuma vikosi huko.

Tayari Umoja wa Mataifa una askari 17,000 wa kuhifadhi amani, ikiwa ndiyo idadi kubwa popote duniani na hadi sasa hakuna amani yoyote wanayofanikiwa kuhifadhi.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vimeshindwa hata kuwalinda raia wala kupata ufumbuzi wa mgogoro huo. Ni kwa sababu hio ndipo sasa juhudi za kidiplomasia badala ya kijeshi zimetia kasi.

Pamoja na kua mgogoro huo una ukabila, vilevile kuna tamaa ya mapato yanayotokana na madini. Rwanda haina utajiri kama wa jirani yake wala ardhi yenye rutuba.

Congo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini -kama dhahabu, alimasi, shaba, chuma na coltan inayotumiwa kwa kutengeneza simu za mkononi.

Utajiri huu wa madini ndiyo unaochagiza na kugharimia vita. Uingereza itatumia ushawihi wake kwa utawala wa Rwanda kuitaka imshawishi Generali Nkunda. Hata hivyo Rwanda inakanusha kua haina uhusiano na Nkunda wala haina uwezo wa kumwambia afanye nini.

No comments: