Monday, September 29, 2008

Denti Akamatwa na Shahada


MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Rebu wilayani Tarime amekamatwa kwa tuhuma za kuuza shahada tano za kupigia kura ikiwemo ya kwake mwenyewe. 

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Oparesheni Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Bw. Venance Tossi katika mkutano na waandishi wa habari ilisema mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Mahemba Daudi (18) alikamatwa saa nne asubuhi alipokwenda kuuza shahada hizo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime. 

Bw. Tossi alisema baada ya vijana wa CCM kumkamata, walimfikisha kituo cha Polisi ambako alifunguliwa shitaka la jinai la kutaka kuuza shahada kinyume cha sheria. 

"Tumemhoji mtuhumiwa kujua shahada zimemfikiaje, mpaka sasa nimeshatuma timu ya wapelelezi kufuatilia ili tujue nani walimtuma au kama zimeibwa,” alisema Kamanda Tossi na kuongeza kwamba "Endapo itabainika, basi yeye pamoja na watakaohusishwa na tukio hilo watapelekwa haraka mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.” 

Alipoulizwa kuwa kijana huyo ni mfuasi wa chama gani, Kamanda Tossi alijibu kuwa kazi ya Jeshi la Polisi si kujua hilo bali kwa vile shahada si mali ya chama chochote, ila cha muhimu ni kuwakamata watu wote wanaofanya biashara hiyo ya kuziuza kwani ni kosa la jinai. 

“Anayeuza shahada na anayenunua wote wanafanya kosa la jinai, wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watamwona yeyote akiuza shahada,” alisema Kamanda Tossi. 

Kamanda Tossi alisema kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilikuwa halijapata taarifa kutoka chama chochote kulalamikia biashara ya uuzaji shahada. 


No comments: