Monday, October 27, 2008

Bunge Kenya lataka tume ya maridhiano

Bunge la Kenya limepitisha muswada wa kuanzishwa tume ya ukweli, haki na maridhiano (TJRC), kuchunguza visa vya kukiukwa kwa haki za binadamu tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru, mwaka 1963.

Wale ambao itathibitishwa walihusika katika visa vya mauaji ya watu wengi na kukiuka haki nyinginezo za kibinadamu kamwe hawatapata fursa ya msamaha.

Hatua hiyo imeafikiwa huku kukiwa na mjadala ni vipi nchi hiyo itakabiliana na wale ambao walihusishwa na ghasia zilizozuka mara tu baada ya uchaguzi uliozusha utata mwezi Desemba mwaka 2007.

Tume ya kimataifa imehimizwa kuwafungulia mashtaka waliohusika katika kupanga ghasia hizo.

Zaidi ya watu 1,500 waliuawa, na wengine zaidi ya 300,000 kuyakimbia makao yao kutokana na mapigano yaliyozuka.

Rais Mwai Kibaki, na kiongozi wa upinzani wa Orange Democratic Movement, Raila Odinga, ambaye sasa ni waziri mkuu, walitia saini makubaliano ya serikali ya uongozi wa pamoja mwezi Februari, katika juhudi za kukomesha ghasia hizo.

Kuanzishwa kwa tume ya maridhiano (TJRC) ni kufuatia mapendekezo ya tume nyengine iliyoanzishwa kuchunguza kiini hasa cha kuzuka kwa ghasia na machafuko hayo ya kisiasa.

No comments: