Wednesday, October 29, 2008

Jaji Lubuva Astaafu, Aipongeza Serikali

Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva ameipongeza serikali kwa kudumisha utawala wa sheria na kuipa nafasi Idara ya Mahakama kufanya shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa na chombo kingine katika mihimili mitatu ya dola. 

Hayo aliyasema jana katika kikao maalumu cha kumuaga katika Ukumbi Namba Moja wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam na kuongozwa na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani pamoja na majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, mahakimu, mawakili na wanasheria. 

Jaji Lubuva alisema katika Katiba ya nchi, suala la mgawanyo wa madaraka limefafanuliwa vizuri ikiwa ni pamoja na mamlaka na nguvu ya kila mhimili ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama yenyewe. “Ni matumaini yangu kwamba kama mihimili hii mitatu ikiwajibika kwa nafasi yake kwa kuzingatia mipaka ya kazi kwa mujibu wa katiba ni dhahiri Mahakama na Mahakama ya Rufaa zitasimamia vizuri utekelezaji wa sheria katika kutoa haki,” alisema Jaji Lubuva. 

Pia Jaji Lubuva aliwataka mawakili kufanya kazi kwa kuzingatia mipaka ya maadili ya taaluma yao. Naye Jaji Mkuu Ramadhani alimsifu Jaji Lubuva ikiwa ni pamoja na kuelezea historia yake kuanzia enzi za chuoni mpaka hapo alipo sasa. “Niliwahi kukutana na Lubuva supermarket na akaniuliza vipi masomo yako, nilishangaa sana kwa sababu sikujua amejua kuwa nasoma, ila alinijibu tu nimeona paper yako, kwa kweli alikuwa ni mtu mzuri na mwenye kusaidia,” alisema Jaji Mkuu. 

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Dk. Fauz Twaib, mbali na kutaja baadhi ya kesi ambazo zimeshawahi kusimamiwa na Jaji Lubuva, pia alisema ametoa mchango mkubwa katika kusimamia sheria. Dk. Twaib alimkaribisha Jaji Lubuva kujiunga katika chama chao ili kufanya kazi kwa kujitegemea. “Maarifa na hekima zake bado zinahitajika sana katika taaluma yetu, tumependekeza amalize kazi kama jaji kwa kujiunga na chama cha mawakili,” alisema Dk. Twaib. Jaji Lubuva alizaliwa Kondoa mwaka 1940 na kufanya kazi kama mtumishi wa mahakama kwa miaka 15.

No comments: