Thursday, November 20, 2008

Pinda Akiri Mgomo wa Walimu Umeyumbisha Nchi


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alitoboa ukweli wa athari zilizoipata serikali aliposema kuwa mgomo wa walimu umeiweka serikali mahali pabaya na kufafanua kuwa kelele zao ziliiyumbisha nchi.

Pinda ambaye ni kinara wa shughuli za serikali pia alitoa kauli iliyoashiria kuwa kiini cha mgomo wa walimu ni utendaji usio wa kuwajibika wa watendaji wa ngazi za chini wa serikali na amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha tatizo hilo halitokei tena na kuifedhehesha serikali.

Kauli ya Waziri Mkuu imekuja siku moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Phillemon Luhanjo kutoa tamko la serikali akiwashukuru "maelfu kwa maelfu ya walimu nchi nzima" kwa kukataa "kushiriki mgomo usiokuwa na kikomo ulioitishwa na Chama cha Walimu (CWT) chini ya Mwenyekiti wake, Gratian Mukoba".

Luhanjo alitoa tamko hilo siku ambayo walimu walikuwa waanze kugoma baada ya kushinda rufaa dhidi ya amri ya kuzuia mgomo iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa Alhamisi ya Novemba 13. Hata hivyo, mgomo huo ulianza huku kukiwa na utata baada ya Mahakama ya Kazi kutoa amri nyingine ya kuuzuia katika hukumu iliyotolewa usiku wa Novemba 17 baada ya serikali kurekebisha maombi yake ya kutaka mgomo huo uzuiwe.

Shauri hilo la serikali dhidi ya CWT litasikilizwa kesho na Mahakama ya Kazi, lakini walimu wamesema baada ya hapo, mgomo utaendelea kama ilivyopangwa.

Jana, Waziri Pinda alitofautiana kabisa na pongezi za Luhanjo akikemea na kuagiza watendaji wa halmashauri kutorudia tena uzembe uliosababisha kuwepo na malimbikizo makubwa kiasi hicho.

Waziri Pinda, ambaye katika ziara yake mkoani hapa aliulizwa juu ya mgomo huo, lakini akakataa kuuzungumzia kwa maelezo kuwa atatoa kauli baada ya mgomo kutokea, jana alionekana kuzungumza kwa uchungu sana na kukiri kuwa nchi iliwekwa mahali pagumu sana.

"Nchi itayumba kwa ajili ya kelele za walimu," alisema Waziri Pinda ambaye alikuwa akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Dodoma.

Pinda alionya kuwa walimu waliiweka serikali mahali pagumu sana na kuwafanya viongozi kufanya kazi kwa nguvu nyingi na kwamba kama kungekuwa na umakini, mambo hayo yasingeweza kutokea.

“Ninakuagiza (Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, William) Lukuvi, kwa niaba ya wakuu wengine wote nchini... hakikisheni kuwa watendaji wenu wa ngazi ya chini wanakuwa makini, ili kusiwe na malimbikizo ya madeni ya walimu kwa kuwa madeni yanaiweka serikali mahali pagumu sana na kwa kweli ni aibu sana.”

Pinda alisema watendaji hawana budi kuhakikisha kuwa malipo ya walimu hayalimbikizwi kiasi cha kuwa mzigo kwa taifa na kuwaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha wanawasimamia watendaji wa ngazi za chini ili wawe makini katika kuzuia madeni ya walimu na kuzuia tatizo kama hilo lisijirudie.

Walimu wanataka kugoma ili kuishinikiza serikali kuwalipa zaidi ya Sh16 bilioni ambazo ni malimbikizo ya malipo yao mbalimbali, lakini serikali imekuwa ikijitetea kuwa ilishalipa zaidi ya nusu ya madai hayo; kuwa madai mengi ni ya kughushi; inaendelea na zoezi la uhakiki.

Katika kuonyesha kuwa mgomo huo uliiyumbisha nchi, serikali imekuwa ikitumia kila mbinu kuhakikisha inazima jitihada za walimu kugoma na kuijeruhi serikali.

Wakati zikiwa zimesalia siku chache kabla ya siku 60 za notisi ya mgomo iliyotolewa na CWT kuisha, serikali ilikimbilia mahakamani na kufanikiwa kuuzuia mgomo huo usianze Oktoba 15 kwa amri iliyotolea na Jaji William Mandia jioni ya Oktoba 13.

Lakini CWT ikafanikiwa kutengua amri hiyo ilipokata rufaa Mahakama ya Rufaa Novemba 13 na kutangaza kuwa mgomo ungeanza tena Jumatatu ya Novemba 17. Lakini siku hiyo, shauri la serikali lilisikilizwa hadi Saa 3:49 usiku wakati Mahakama ya Kazi ilipotoa amri ya kuuzuia tena mgomo huo usiendelee Novemba 18 baada ya serikali kurekebisha maombi yake ya amri hiyo ya muda ya kusitisha mgomo.

Wakati maofisa wa serikali wakihaha mahakamani, maofisa wengine walikuwa wakihaha kuandaa malipo ya madai ya walimu hao na Jumapili ya Novemba 16, serikali ilitoa tangazo kuwa malipo yote yameshatumwa kwenye halmashauri huku ikiwasihi walimu wasianze mgomo Novemba 17 kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, malipo hayo yanaonekana kuwa huenda yakawa chanzo cha matatizo mengine baada ya walimu kutoka mikoa kadhaa kuripotiwa kupunjwa malipo yao, huku wengine wakikuta malipo hewa.

Katika ziara yake mkoani Dodoma, mbali na kuwataka watendaji kuwa makini katika kushughulikia malipo ya walimu , Waziri Pinda amekuwa akizungumzia kwa nguvu utendaji wa watendaji hao, akiwataka wabadilike na kuwajibika kwa wananchi.

Katika hotuba yake ya majumuisho Waziri Pinda aliwataka viongozi kuwa na mikakati ya kudumu katika kuondoa kero kwa wananchi na kushirikiana na serikali katika kutatua matatizo makubwa yanayotokea hapa nchini.

Aliagiza kuwepo na mahusiano mazuri kati ya serikali kuu na serikali za mitaa, akisema kuwa zote zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi na ni sehemu ya serikali moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mkuu pia alirudia kauli yake ya kuwataka Watanzania kuondoka wakijua kuwa vita kuu iliyo mbele yao ambayo wanapaswa kupigana nayo ni vita ya kilimo ambayo walisema kuwa, ni lazima kila mtu kuvaa silaha za kivita na kuingia msituni kwenda kupigana.

Aliwaagiza viongozi kutokaa ofisini na badala yake waende kwa wananchi kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi mara moja, huku akisisitiza kuwa kila mkoa ni lazima kuwe na daftari la kudumu la kilimo.

Kuhusu wakuu wa wilaya aliwaagiza kufanya mikataba na viongozi wao wa ngazi za chini, wakiwemo watendaji wa kata na vijiji, akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Wilaya ya Chamwino ambaye amefanikiwa katika ujenzi wa shule za sekondari wilayani mwake baada ya kuwekeana mikataba na watendaji wake.

No comments: