Tuesday, November 4, 2008

Walinzi Wauawa Wakiwa Lindoni

Walinzi wawili wameuawa katika wilaya za Pangani mkoani Tanga na Musoma Mkoa wa Mara, katika matukio ya mauaji yaliyotokea mwishoni mwa wiki wakiwa lindoni. Wilayani Pangani, mtu aliyetambuliwa kuwa ni Enock Kisali (33), mlinzi katika shamba la mkonge la Mwera Estate lililopo Kijiji cha Tungamaa wilayani humo, ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali ubavuni na watu wasiojulikana. 

Akithibitisha mauaji hayo ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Simon Sirro, alisema tukio hilo lilitokea Novemba mosi, mwaka huu majira ya usiku wakati marehemu akiwa lindoni kwake. Alisema Novemba 2, mwaka huu, majira ya saa 5.00 za asubuhi Polisi wilayani humo walipata taarifa kutoka kwa raia wema waliouona mwili wa Kisali ukiwa umetelekezwa kichakani karibu na shamba hilo. 

Alisema baada ya Polisi kupekua mwili huo, walibaini kwamba marehemu alichomwa na kitu hicho chenye ncha kali na pia alikuwa amenyongwa shingo. Alisema chanzo cha kifo hicho hakijafahamika. Wilayani Musoma, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumchinja mlinzi wa Kimasai aliyekuwa akilinda duka la mfanyabiashara Crismas Manyama. 

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Mara, Deus Kato alisema tukio hilo limetokea juzi usiku katika eneo la Bweri nje kidogo ya Mji wa Musoma, likimhusisha Emmanuel Rembu (30). Kato alisema mlinzi huyo alichinjwa na kwamba baada ya mauaji hayo, majambazi hao waliumwagia ukuta wa duka hilo maji ambayo yaliwarahisishia kazi ya kubomoa matofali kisha kuingia ndani na kupora vitu mbalimbali ambavyo thamani yake haijajulikana. Kaimu Kamanda huyo ambaye pia ni Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Mara alisema maiti ya mlinzi huyo ilitelekezwa na kukutwa asubuhi yake na watu waliokuwa wakipita maeneo hayo wakienda katika shughuli zao za kila siku. Hakuna aliyekamatwa hadi sasa.

No comments: