KAMPUNI ya Kuhudumia Makontena Bandarini (TICTS), imesema itasimama imara kuhakikisha Tanzania inapata medali katika Michezo ya Olimpiki itakayofanyika London, 2012.
Hayo yalisemwa na Meneja Masoko wa TICTS, Predi Asenga, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo, katika hafla fupi ya kukabidhi bendera na kuwapongeza wanamichezo hao kwa kudumisha nidhamu katika michezo hiyo.
Asenga alisema wanamichezo wa Tanzania walikumbana na ugumu wa michezo kutokana na kukutana na wanamichzo walio na maandalizi ya nguvu, lakini ana imani kwa kadri TICTS watakavyoingia kwenye timu ya 2012, medali zitapatikana.
“Tunataka kufanya maandalizi ya muda mrefu, lazima Tanzania tuibuke na medali michezo ya London, lakini yote ni maandalizi, TICTS tunaliweza hilo na tutahakikisha Tanzania inaweka historia,” alisema.
Wanamichezo wa Tanzania walifanya vibaya katika michezo ya Olimpiki ya Beijing, ambapo kati ya wanamichezo wanane, hakuna hata mmoja aliyeibuka na medali.
''Tuna matumaini, ushirikiano wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), fedha zaidi zinaweza kupatikana kwa ajili ya kuwasaidia wanamichezo wetu, katika michezo ijayo kuelekea michezo ya Olimpiki ya London 2 012. Tutafanya kila tuwezalo kuunga mkono juhudi hizo kwa njia yoyote ile tutakayoweza.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa, BMT, Kanali mstaafu Idd Kipingu, ameipongeza TICTS, hasa kwa kufanimkisha ushiriki wa Tanzania katika michezo hiyo ya Beijing China.
Hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha mchana kwa msafara wa wanamichezo wa Olimpiki ukijumuisha waogeleaji pamoja na wanariadha, iliandaliwa na serikali kwa kushirikiana na TICTS, kwenye hoteli ya Travertine, jijini Dar es Salaam.
Kipingu alisema, TICTS ni wapya katika medani ya michezo na kuwa kwa niaba ya serikali, akiwa kama Mwenyekiti wa BMT wanawapongeza na kuwakaribisha katika udhamini wa michezo nchini.
''Hatukupenda mlivyoitwa watalii, tena wengi wao ni Waandishi wa Habari, lakini nasikitika hawakujua nini maana ya Olimpiki, kuna mambo mengi huko ambako walimu, wachezaji wamejifunza…,'' alisema.
Naye Rais wa TOC, Ghulam Rashid, aliahidi kukaa pamoja na kujipanga kwa kuangalia upungufu uliojitokeza katika mashindano ya mwaka huu na kuanza mapema maandalizi ya michezo ijayo ya London 2012.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment