Monday, September 15, 2008

Bibilia yamponza Makamba

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yussuf Makamba amesema tabia yake ya kunukuu Kitabu cha Biblia ndiyo iliyomponza na kunukuliwa vibaya na vyombo vya habari kuhusu suala la Nape Nnauye kwamba hawezi kukata rufaa baada ya kufukuzwa. 

Akikanusha kauli yake aliyoitoa hivi karibuni kuhusu Nape akidai kuwa ``amefungiwa Mbinguni na Duniani`` akimaanisha kuwa hawezi kukata rufaa popote alisema, yeye hakumaanisha hivyo. 

``Unajua siku zote waandishi wa habari, wanajua kuwa napenda sana kunukuu baadhi ya vifungu vya Biblia hivyo na siku hiyo nilipoulizwa suala hilo nikazungumzia kama utani, sikujua kama wenzangu `wamenikoti` `` alisema Makamba. 

Alisema Nape hawezi kufukuzwa NEC kwa vile haingii kwenye nafasi hiyo kupitia umoja wa vijana na wenye mamlaka ya kumwondoa ni Halmashauri Kuu. 

Alisema Halmashauri Kuu haiwezi kuingilia maamuzi yaliyochukuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Vijana kwa vile wanakanuni zao zinazowaruhusu kwa mujibu wa katiba ya umoja wao. 

Alisema katiba ya chama hicho haisemi wazi kuwa mjumbe wa NEC anapovuliwa unachama na jumuiya yake, anakuwa ameondolewa kuwa mjumbe wa mkutano huo au la. 

No comments: