“HUU si ushindi wangu binafsi, bali ni ushindi wa Watanzania. Ni ushindi wa wazalendo wa nchi hii, dhidi ya mafisadi. Hakika, huu ni ushindi wa wananchi wazalendo wa kweli katika taifa lao.
“Ni ushindi wa wanademokrasia, dhidi ya wahujumu wa demokrasia. Ni ushindi wa wanyonge, dhidi ya wachafuzi wanyonyaji wa taifa.”
Haya ndio maneno anayosema mbunge wa Karatu (CHADEMA), mkoani Arusha Dk. Willibrod Slaa, kuelezea hisia zake baada ya kushinda kesi aliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga ubunge wake katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Jaji Makaramba katika uamuzi wake alifika mbali zaidi. Alisema “Mahakama imekubaliana na hoja za wakili wa utetezi Tundu Lissu, kwamba walalamikaji waliwasilisha nyaraka za kughushi.”
Uamuzi huo umemkosha Dk. Slaa. Hata hivyo, anasema kwamba alitarajia kushinda. “Sikuwa na mashaka na kesi hii. Madai ya walalamikaji hayakuwa na nguvu za kisheria,” anafafanua.
Anasema, “Wenzetu walighushi nyaraka. Walikuja mahakamani na nyaraka za uwongo. Walikuja na madai ambayo huwezi kuyathibitisha mbele ya mahakama.”
“Kimsingi walikuja kuidanganya mahakama. Bahati njema mahakama imeuona uwongo wao. Katika mazingira hayo, hata kama Jaji angetaka kuwabeba asingeweza, maana walikuwa hawabebeki,” anafafanua.
Pamoja na kwamba kesi hiyo imefunguliwa na wanachama watatu, Dk. Slaa anaamini kuwa mshindani wake katika uchaguzi huo, Patrick Tsere ndiye aliyekuwa anaifadhili.
Kwa nini? Anasema, “Kila kesi ilipokuwa inatajwa bwana huyu alikuwa anashinda katika viwanja vya mahakama. Alikuwa anatumia muda mwingi katika kesi ile, kuliko kufanya kazi za umma.”
“Ni kweli alitakiwa mahakamani kuja kutoa ushahidi. Alikuja mara moja na kumaliza kazi yake.
Lakini kila mahakama ilipokuwa inakutana, Tsere naye alionekana katika viwanja vya mahakama. Hii ina maana kwamba pamoja na kuwa kesi ilifunguliwa na wengine, lakini yeye alikuwa amejificha nyuma yao.”
“Ufisadi upo wa aina nyingi. Kuna watu wanaibia serikali kwa kuchota mabilioni ya umma, na wengine wanalipwa bila ya kufanya kazi. Hawa wote ni mafisadi,” anasema kwa hali ya kuchukia.
Anasema, “Katika hili, Tsere anakuwa fisadi kwa kuacha kazi za serikali na kushinda mahakamani bila sababu za msingi.” Katika uchaguzi huo, Dk. Slaa alimshinda Tsere. Kwa sasa Tsere ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.
Mbali na Tsere, Dk. Slaa anamtaja Martin Thomas, kwamba alikuwa mmoja wa wafadhili wakuu wa kesi hiyo. “Huyu aliomba tenda ya ujenzi wa barabara wilayani Karatu. Baraza la Madiwani la Halmashauri, ikamfuta baada ya huko nyuma kujenga madaraja yasiyofikia kiwango,” anasema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment