Friday, September 19, 2008

Kikwete Amtembelea Athumani Hospitali


RAIS Jakaya Kikwete jana alimjulia hali Mpigapicha Mkuu wa gazeti hili, Athumani Hamisi, ambaye amelazwa katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) Dar es Salaam, baada ya kupata ajali ya gari wiki moja iliyopita mkoani Pwani. 

Rais Kikwete na msafara wake alifika hospitalini hapo saa 11:20 jioni na moja kwa moja alikwenda kwenye chumba alicholazwa mwanahabari huyo na kumjulia hali, huku akieleza wazi kusikitishwa na ajali iliyompata. 

“Athumani, nimesikia kwamba umepata ajali, nimesikitishwa sana…nimekuja kukuona, nitazungumza na madaktari kuona nini cha kufanya,” ilikuwa kauli ya Rais Kikwete kwa mfanyakazi huyo wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN), inayochapisha pia magazeti ya Daily News na Sunday News. 

Rais Kikwete alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Profesa Lawrence Museru pamoja na Mhariri Mtendaji wa TSN, Isaac Mruma. 

Athumani alipata ajali Ijumaa iliyopita majira ya saa tatu asubuhi eneo la Kibiti mkoani Pwani akiwa njiani kwenda Kilwa mkoani Lindi, kwa ajili ya kuripoti matukio ya Taasisi ya Vodacom Foundation kufuturisha watoto wa mjini humo. 

Mpigapicha huyo alikuwa na wenzake wawili, Heri Makange wa Channel Ten na Anthony Siame wa New Habari Corporation, ambao hata hivyo, hawakuumia sana kulinganisha na Athumani ambaye ameumia sehemu za kichwani na kifuani

No comments: