Wednesday, September 10, 2008

Sumaye amtetea Nape

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameeleza kushangazwa na kushtushwa na uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana la Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa kumpokonya uanachama wake, Nape Nnauye.

Sumaye alisema uamuzi wa kumwadhibu Nape wakati akiwa mgombea wa uenyekiti wa UVCCM unaweza kutafsiriwa kuwa ni jitihada za makusudi zilizofanywa na maadui zake kisiasa.

“Mimi sina hakika sana na haya ninayoyasoma kwenye vyombo vya habari, lakini kama baraza lingeamua kujadili majina, basi lingeshughulika na majina ya wagombea tu, na kama lingetaka kujadili kauli ya Nape kuhusu tuhuma alizotoa, basi lingefanya hivyo, kwani unapozichanganya hoja zote kwa wakati mmoja, lazima watu watahoji, kama ilivyo sasa,” alisema Sumaye.

“Kama kweli Makamba amesema yanayosemwa kwenye vyombo vya habari, maana wakati mwingine magazeti yetu yanaongeza chumvi, lakini kama ni kweli, nadhani hizo si kauli za mtu anayepaswa kuwa kiongozi wa chama chetu,” alisema Sumaye bila kutaka kuingia kwa undani juu ya suala hilo.

Sumaye amesema anakusudia kueleza dukuduku lake hilo kuhusu uamuzi huo wa UVCCM wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) inayokutana mjini Dodoma leo.




No comments: