Wednesday, September 17, 2008

Tz Yapata Msiba Mwingine Kutoka Ugenini

Wafanyabiashara wawili raia wa Tanzania, wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Burundi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi na kuporwa kila kitu walichokuwa nacho. 

Habari kutoka kwa ndugu wa marehemu hao, zilidai kuwa Watanzania hao waliuawa juzi jioni mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Kijiji cha Kabonga walipokuwa wakivuka mpaka kutoka Burundi kuingia Tanzania, mwambao wa kaskazini mwa Ziwa Tanganyika. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, ndugu huyo wa marehemu, Shaaban Juma aliwataja waliokufa kuwa ni Kibona Salehe Mwenge (32) mkazi wa Ujiji Mjini Kigoma na Bahati Soud au Mama Masoud mkazi wa Kilimahewa mjini hapa. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Abdihaki Rashid amekiri kuwapo kwa tukio. Hata hivyo, alisema hana taarifa zozote zaidi za jinsi mauaji hayo yalivyotokea na anasubiri kuletewa taarifa na watu wake. Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Joseph Simbakalia alipopigiwa simu na waandishi wa habari jana kuhusu taarifa zaidi za tukio hilo, alisema apigiwe Kamanda Rashid ambaye ndiye mwenye taarifa zote. 

No comments: