Saturday, September 20, 2008

Watoto Wa Vigogo Mahabusu

WATOTO wa vigogo wanaofanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wameburutwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kughushi vyeti vya sekondari. 

Washitakiwa hao walifikishwa jana mahakamani hapo na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCB) na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Bibi Neema Chusi. 

Watuhumiwa hao ni Bi Justina Mungai, Bi Christina Ntemi, Bi Siamini Kombakono, Bi Janeth Mahenge, Bi Beatha Masawe, Bi Jacqueline Juma, Bi Philimina Mutagurwa na Bi Amina Mwinchumu. 

Akisomewa mashitaka, mshitakiwa wa kwanza, Bi Justina alidaiwa kuwa mwaka 2001 alighushi cheti cha sekondari namba S.342/43 cha Februari 26, 1980 akionesha kuwa kimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania. 

Alidaiwa kuwasilisha cheti hicho katika Benki hiyo huku akijua kuwa ni cha kughushi. 

Mshitakiwa wa pili, Bi Christina alidaiwa kuwa mwaka 2002 alighushi cheti na kukiwasilisha BoT ambacho ni namba S.0222/42 cha Novemba 1999. 

Ilidaiwa kuwa Bi Siamini alighushi cheti namba S.238-0076 cha Machi 14 mwaka jana na kukiwasilisha BoT akionesha kimetolewa na Baraza la Mitihani. 

Naye Bi Janeth alidaiwa kughushi cheti namba S.311/0071 cha Machi 14, 1997 ambacho alikiwasilisha BoT huku Bi Beatha akidaiwa kughushi cheti namba S.331/0071 cha Aprili 2000 na kukiwasilisha katika benki hiyo. 

Washitakiwa wengine ni Bi Jacqueline ambaye anadaiwa kughushi cheti namba S.375/020 cha Machi 14,1999, Bi Philimina cheti namba S.0764/0012 cha Machi 1997. 

Mashitaka ya mwisho yalimkabili Bi Amina ambaye alidaiwa kughushi cheti namba S.0307/004 cha Machi, 1991 na kukiwasilisha katika benki hiyo huku akijua kuwa ni cha kughushi. Wote walikana mashitaka. 

Upelelezi umekamilika na dhamana iko wazi ambapo mahakama iliwataka kuwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi wa Serikali, hata hivyo hawakukamilisha masharti ya dhamana na hivyon kurudishwa ndani. Kesi itakuja tena Oktoba 6 mwaka huu.

No comments: