Tuesday, September 30, 2008

Watalii Waliotekwa Waachiwa Huru


Kundi la watalii kutoka nchi za magharibi na waongozaji wao wenye uraia wa Misri waliotekwa nyara siku 10 zilizopita wameachiliwa huru.

Mateka hao 11 wakiwemo Waitaliano watano, Wajerumani watano na raia mmoja wa Romania na waongozaji wao wameripotiwa kuwa katika afya njema.

Kundi hilo lililotekwa nyara katika mji mmoja mpakani mwa Misri kwa sasa wanaelekea mjini Cairo.

Wakati wa utekaji nyara huo watu hao walizungushwa katika eneo la jangwa lisiloruhusiwa kupitwa lililosambaa maeneo ya Misri, Sudan, Libya na Chad.

Hatua ya kuachiliwa huru kwa watu hao ulitangazwa katika televisheni ya taifa ya Misri na kuthibitishwa na wizara ya mambo ya nje ya Italia.

Watekaji nyara hao walitaka Ujerumani ilipe fidia ya dola za kimarekani milioni 8.8.

Haijajulikana wazi iwapo fidia hiyo ililipwa.

No comments: