Sunday, September 28, 2008

Watoto Afrika Wakutana Dar


Watoto kutoka nchi tisa za Afrika wako Dar es Salaam kuhudhuria mkutano kwa ajili yao juu ya changamoto wanazopata watoto wanaoishi katika mazingira magumu na ukubwa wa tatizo la Ukimwi. 

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Fatma Mrisho, alisema Dar es Salaam jana kuwa hisia, mitazamo na mahitaji ya watoto wa Afrika vitawasilishwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Rais Jakaya Kikwete atakayewahutubia watoto hao kesho. 

“Watoto wana tatizo la kipekee lakini lazima tukae tuone kuna haja ya kuboresha mtazamo wetu,” alisema Dk Mrisho na kueleza kuwa huenda tatizo la Ukimwi kwa watoto lina sura tofauti na ile inayofahamika katika jamii. 

Mmoja wa watoto wanaoiwakilisha Tanzania katika mkutano huo siku mbili, Nyabuchwenza Methuseka alisema, jamii inapaswa kuwajali watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wapate elimu. Mwezeshaji Mkuu wa mkutano huo, Richard Mabala alisema, watoto wanaohudhuria wanatoka Burundi, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Ethiopia, Zambia, Kenya, na wenyeji Tanzania.

No comments: