Friday, September 26, 2008

Zombe Wamtosa


MKUU wa Upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake 12, ameieleza Mahakama Kuu kuwa karibu watuhumiwa wote walipotakiwa kuandika maelezo yao kwa mara ya pili, walimgeuka Zombe. 
Askari wasiokwenda msitu wa Pande walikuwa watatu ambapo mmoja kati yao shahidi huyo alidai hamkumbuki. 

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Majura Magafu mbele ya Jaji Kiongozi, Salum Massati, Mkumbi ambaye ni shahidi wa 36, alidai watu hao walikamatwa Sinza Palestina Block C kwa utaratibu bila mashambulizi na kwenda kuuawa katika msitu huo. Pia hawakuwa majambazi na hawajahusika na wizi wa kampuni ya Bidco. 

“Wao waliungana na wenzao na kudanganya katika maelezo yao kuwa waliouawa walikuwa majambazi na waliiba Bidco wakati si sahihi,” alidai. Hata hivyo, Jaji Massati alipomhoji shahidi kwa namna gani askari wadogo walihusika katika tukio hilo wangewezaje kuzuia matukio ya Sinza na katika Msitu wa Pande yasitokee, Mkumbi alijibu “walitakiwa baada ya kutoka katika msitu wa Pande immediately (haraka) waripoti tukio hilo kwa ofisa yeyote wa polisi.” 

Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Magafu na shahidi huyo wa 36 ambaye ni Mpelelezi Mkuu katika kesi inayomkabili Zombe na wenzake 12, Sydney Mkumbi yalikuwa kama ifuatavyo: 

Wakili: Unafahamu washitakiwa wanakabiliwa na nini? 

Shahidi: Nafahamu, kosa la mauaji Wakili: Wapi? Wakili: Katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luisi. 

Wakili: Zombe alikuwapo? Shahidi: Hakwenda msituni. Wakili: Zombe alikuwapo Sinza wakati marehemu wanakamatwa? Shahidi: Hakuwapo. Wakili: Imedaiwa kulikuwepo mapambano kati ya marehemu na askari katika ukuta wa Posta huko Sinza, je, Zombe alikuwepo? Shahidi: Kwenye mapambano hakuwepo. 

Wakili: Ukiachilia mbali maelezo ya Rashidi kuwa Zombe aliwasiliana na mshitakiwa wa pili yaani Christopher Bageni, kuna sehemu Zombe amehusishwa? Shahidi: Mshtakiwa namba mbili aliandika barua kwa DCI akitaka Tibaigana awepo. Wakili: Unayo? 

Shahidi: Sina hapa? Wakili: Jana hukusema. Shahidi: Ningeulizwa ningesema. Wakili: Umezua leo asubuhi hii. Shahidi: Wewe ndiyo umezua? Wakili: Katika upelelezi wako, kuna sehemu uligundua watuhumiwa walikaa pamoja wakasuka njama za kuwaua hao marehemu? Shahidi: Kwa mtiririko ulivyo walikuwa pamoja, walikutana Block C na wakasema ‘tumeamriwa tukachinje’ 

Wakili: Waliwasiliana? Shahidi: Ndiyo kwa simu ya upepo na mawasiliano ya simu ya mkononi. 

Wakili: Unazifahamu simu za Zombe na Bageni? Shahidi: Nilikuwa nazijua lakini sasa sizijui tena. Wakili: Ulienda kufuatilia mazungumzo yao katika ofisi za simu? Shahidi: Nilifanya hivyo, niliagiza kwa maneno Wakili: Ulipata majibu? 

Shahidi: Nilipata majibu kuwa muda ulishapita kwani Vodacom wanatunza maongezi kwa miezi sita halafu wana destroy. Wakili: Kuua ni amri halali? 

Shahidi: Si amri halali. Wakili: Nikiwa na bosi wangu nikamuona anaiba nami ntakuwa nimefanya kosa? Shahidi: Utawajibika, kwa nini usizuie wizi usitendeke? 

Wakili: Akiwa na silaha mimi sina je? Shahidi: Ungetakiwa uripoti ofisa fulani ametenda kosa ukinyamaza unahusika. Wakili: Kuna malalamiko askari walichukua pesa za marehemu. 

Shahidi: Nilisikia, lakini hilo ni kosa la wizi Wakili: Mtu anaweza kuuawa pasipo sababu? Shahidi: Inawezekana. Wakili: Swali langu la msingi sasa linasema ili uweze kumwua mtu lazima uwe na chuki naye kama si bahati mbaya? Shahidi: Lazima sababu iwepo. 

Wakili: Washtakiwa walikuwa wakifahamiana na marehemu? Shahidi: Hawafahamiani. Wakili: Unakubaliana nami kama si tukio la Bidco wasingekutana? 

Shahidi: Ni kweli. Wakili: Katibu wa Tume ya Kipenka alikuambia washtakiwa walipora pesa? Shahidi: Sikumhoji. 

Wakili: Hapa mahakamani imedaiwa sababu ya wale kuuawa ni askari walipora pesa, ulifahamu? Shahidi: Nilifahamu baadaye. Wakili: Hadi sasa hufahamu? 

Shahidi: Nafahamu kwa sababu ya ushahidi wa kina Lunje Wakili: Si mliwapandikiza? Shahidi: Nafsi iliwasuta. Wakili: Mlipewa kazi nzuri, lakini mlikuwa biased Shahidi: Uliza swali Wakili: Uliwahi kumuuliza Bageni begi la pesa lilikwenda wapi? Shahidi: Sikumhoji. 

Wakili: Rashidi na Rajabu hawakuwa wakweli, unasemaje? Shahidi: Walikuwepo katika tukio, hawakukiri kuua walishuhudia mauaji. Wakili: Nani mashahidi? 

Shahidi: Wote waliamriwa kuandika maelezo yao upya, walifuatwa rumande na karibu wote isipokuwa mshitakiwa wa kwanza (Zombe) waliandika maelezo yanayofanana na Rashidi na Rajabu. Wakili: Rashidi alisema walipewa kikaratasi, ni kweli? 

Shahidi: Ndiyo alipewa na akasema ‘hata mke wangu simuachii, ntakuwa nacho mwenyewe’ 

Wakili: Kilikuwa na saini ya mkubwa? Shahidi: Alinionyesha tu na sikuona saini Wakili: Ni mwandiko wa mtu au typing? Shahidi: Kiliandikwa kwa typewriter . Baada ya kuhojiwa na Magafu, 

Mkumbi alihojiwa na wakili Longino Myovela na mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo: Wakili: Kama mpelelezi unaamini Koplo Saad aliua? Shahidi: Naamini 

Wakili: Ungekuwa katika Tume ungewaingiza hawa wengine (watuhumiwa 12) wakati Saad ndo ameua? 

Shahidi: Uchunguzi ungeniongoza. Wakili: Kuwakamata marehemu ni kosa? Shahidi: Si kosa wanatekeleza kazi ya polisi. 

Wakili: Ni lazima junior polisi atekeleze amri ya wakubwa? Shahidi: Ni sahihi kutekeleza amri ya kiongozi Wakili: Kwenda msitu wa Pande kwa amri ni sawa? 

Shahidi: Ni amri halali kwenda msitu wa Pande, lakini utekelezaji wake si halali. Wakili: Zaidi ya kuona Saad akiua, Rashid alikuambia nini? Shahidi: Rashidi alisema Bageni alikuwa anawasiliana kwa simu na kiongozi wake kwa sababu alikuwa akisema ‘afande afande’.

No comments: