Wednesday, October 22, 2008

Dk. Shein aonya matumizi mabaya ya madaraka


Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein ametahadharisha juu ya matumizi mabaya ya madaraka katika halmashauri na kuwataka viongozi na watendaji kuziendesha kwa kuzingatia misingi ya utawala bora. 

“Sheria na kanuni zifuatwe pasiwe na ubabe katika halmashauri na taasisi za serikali, tukifanya hivyo tutakuwa tumezingatia utawala bora,” alisema na kusisitiza kuwa kwa wale ambao wawejisahau hapana budi wakakumbushwa, lakini alionya kuwa pindi wasiposikia wasisite kuchukuliwa hatua zifaazo. 

Dk. Shein alitoa tahadhari hiyo juzi wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Arusha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), akihitimisha ziara yake ya siku saba. 

“Hakuna aliye juu ya sheria, si Mwenyekiti, Mkurugenzi wala diwani wote tunapaswa kufuata sheria na taratibu zinazoendana na madaraka tuliyopewa. Tutekeleze mipango tuliyoipanga katika vikao vyetu kutekeleza wajibu wa kuwatumikia wananchi,” alisema Dk. Shein. 

Alisema halmashauri si mahali ambako kila kiongozi anaweza kuleta ajenda au mipango yake kutekelezwa na kuzitaka kutenda haki katika kuwahudumia wananchi kwa kutoruhusu upendeleo. Katika mkutano huo, Makamu wa Rais aliwakumbusha viongozi wa mkoa huo kutekeleza wajibu wao kwa ushirikiano na kujenga mshikamano na upendo miongoni mwao na kuongeza kuwa uongozi wa pamoja unaepusha kulaumiana miongoni mwa viongozi. 

“Ni muhimu kuimarisha uongozi wa pamoja kwa kushauriana na kuonyesha mshikamano miongoni mwenu na katika mazingira kama hayo hata pale mambo yanapokwenda kombo kila mmoja atasita kumlaumu mwenzake,” alisema na kueleza kuridhishwa na jitihada za viongozi na watendaji katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na juhudi za wananchi wa Arusha katika kujiletea maendeleo. 

Dk. Shein ambaye alitembelea wilaya zote isipokuwa Ngorongoro, hata hivyo, aliutaka uongozi wa mkoa na wilaya kupanga mikakati bora zaidi ya kuimarisha kilimo cha kisasa na ufugaji bora ambao tayari umeonyesha mafanikio katika baadhi ya sehemu mkoani humo. 

Aliwataka viongozi na watendaji wa Mkoa wa Arusha kutekeleza mpango wa uimarishaji wa sekta ya kilimo mkoani humo kwa kuzingatia uongezaji tija kwa kutumia njia bora za kilimo pamoja na matumizi ya mbegu bora na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji

No comments: