Wednesday, October 22, 2008

Vyama vya siasa vyadai mwafaka ni mradi wa CCM na CUF

VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wamevishutumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kuwa wanaendekeza ufisadi kwa kisingizio cha mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar kila unapomaliza uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa National League for Democracy (NLD) Dk Emmanuel Makaidi alidai kusa CCM na CUF hawana ugomvi wowote isipokuwa wana mradi wao wa kifisadi wa

kutafuta fedha kwa kupitia mwafaka.

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo katika warsha ya siku mbili ya viongozi wa kitaifa wa

vyama vya kisiasa nchini inayofanyika katika hoteli ya Bwawani iliyoandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET).

Dk Makaida alisema anashangazwa vyama hivyo kung’ang’ania kutatua wanchodai kuwa ni mgogoro wa Zanzibar pasipo kushirikisha vyama vyengine vya siasa vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria na kusisitzia kuwa visiwani humo hakuna vyama viwili kama ambavyo CCM na CUF wanataka ionekane.

“Kwani nini wanangangania vyama viwili kufanya mazungumzo yasiokwisha na kila baada

ya uchaguzi mkuu wafadhili wanakutana na kutoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo. Huu ni ufisadi…samahani kwa kusema hayo,” alisema Makaidi.

Alisema kitu ambacho hakubaliani nacho ni CUF kuandaa maandamano kudai serikali ya mseto huku wakitambua kuwa wao wana nafasi katika bunge, hivyo walipaswa

kwanza kuwafichua mafisadi wanaorejesha nyuma maendeleo ya nchi.

Mwakilishi wa Chama Cha Sauti ya Umma (SAU), Peter Mwagira alisema kwamba hawakubaliani na mgogoro unaozushwa na CCM na CUF visiwani Zanzibar kwani mgogoro huo ni wa kupika kwa lengo la kuwanufaisha vyama hivyo viwili.

Alisema mgogoro uliopo ni baina ya vyama vyengine vya kisiasa dhidi ya CCM na CUF ambao unatakiwa kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.

Viongozi wengine waliochangai mada hiyo ni Victor Manyai aliyedai kuwa CUF na CCM vinageuza mazungumzo ya kutafuta mwafaka kuwa ni mgodi wao.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha TADEA, Dustan Lifa Chipaka alidai kuwa CCM na CUF walikula njama katika kuharibu mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar na kwamba mchakato wa mazungumzo hayo ni kiini macho.

Wakitoa mada katika warsha hiyo juu ya migogoro na utatuzi wake ndani ya vyama na suluhisho la migogoro baina ya vyama Tanzania, wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Professa Mohabe Nyirabu na Bashiru Ally walielezea udhaifu unaosababisha hali hiyo.

Professa Nyirabu alisema kuwa tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kumekuwa na migogoro mingi na kwamba uhai wa baadhi ya vyama unatatemea nguvu na uwezo wa waanzilishi wake.

Naye Profesa Bashiru alisema kuwa vyama vingi vimeingia katika migogoro baina yao kutokana na kukiuka misingi ya demokrasia na kutoheshimu taratibu walizojiwekea.

No comments: