Monday, October 27, 2008

JK Ataka Walimu Walioghushi Waadhibiwe

Rais Jakaya Kikwete ameagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya walimu ambao wameghushi au kudanganya wanaidai Serikali wakati hawaidai. Rais ametoa agizo hilo baada ya kuona kuna ongezeko la madai ya walimu kila siku wakati Serikali ilikwisha walipa walimu hao Machi mwaka huu kiasi cha Sh bilioni 7. 

Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya Rais Kikwete Alhamisi iliyopita kuagiza kuwa madai yote ya walimu yapitiwe upya na ikibidi viongozi wapite shule hadi shule kubaini nani ana madai halali. 

Akitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Tabora, Rais alionekana kukerwa na taarifa ya Mkuu wa Wilaya hiyo Moshi Chang’a ambaye alisema walimu wa wilaya hiyo wanaidai Serikali. 

“Deni gani hilo lisilokwisha, haiwezekani tunalipa madeni; lakini yanazidi kuongezeka ama kuna tatizo la viongozi au kuna walimu hawana madai halali,” alisema Rais na kutaka sheria kali zichukuliwe dhidi ya wale watakaobainika kudanganya. 

Rais alitaka ufafanuzi wa madeni hayo ndipo Mkuu wa Wilaya hiyo, Chang’a alisema Msingi wanadai Sh milioni 92.5 kwa ajili ya likizo, posho na uhamisho wakati wale wa Sekondari wanadai Sh milioni 191.8. za posho, matibabu, uhamisho, likizo na malimbikizo ya mishahara. 

“Mheshimiwa Rais baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ni pamoja na madeni ya walimu,” alisema Chang’a. Juzi Rais aliagiza kufanyike uhakiki wa madeni ya walimu kuanzia shuleni ili waweze kulipwa haraka. Hivi karibuni walimu walitishia kugoma, lakini mahakama ilizuia mgomo huo kitendo kilichofanya Chama cha Walimu (CWT) wakate rufaa Mahakama ya Rufani.

No comments: