Monday, October 27, 2008

Rostam Aburutwa Kortini


MWANASIASA mashuhuri nchini ambaye pia ni Mbunge wa Igunga (CCM), Bw. Rostam Aziz ameburutwa kortini akitakiwa kulipa mamilioni ya fedha na pia kuomba radhi kwa kile kilichoelezwa kuwa wazazi wake kujihusisha na biashara ya utumwa, limebaini gazeti hili. 

Rostam ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu ya Taifa za CCM, kwa hatua hizo sasa atalazimika kufika Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Kalegeya Novemba 11 mwaka huu kujitetea kutokana na mashitaka hayo. 

Katika kesi ya madai namba 131 ya mwaka huu iliyofuinguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila na Majira kupata nakala yake, Rostam pamoja aliyeunganishwa na magazeti kadhaa nchini yaliyiripoti haba ri hiyo, anadaiwa kumkashifu kiongozi huyo na kutakiwa kulipa sh. bilioni 3. 

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka yenye kurasa 10, vipengele 37 na vielelezo lukuki, Mtikila anadai kuwa Bw. Rostam alimchafulia jina na hadhi yake mbele ya jamii kwa maneno aliyoyasema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari wa Julai 13 mwaka huu, ambao pia uliripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari zikiwemo tovuti na kuibua mijadala kwenye intaneti. 

"Julai 13 mwaka huu mdaiwa wa kwanza (Rostam) katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinski alitoa kauli iliyonidhalilisha," inaeleza sehemu ya hati hiyo. 

Maneno ambayo Mtikila anadai kuwa yalimkashifu, yameanza kubainishwa katika katika kipengele cha 12 cha hati hiyo ya mashitaka ikimkariri Bw. Rostam akisema: 

"Matamshi yaliyotolewa wiki hii na Mtikila ni kinyaa, yananuka harufu ya chuki, wivu,ubaguzi,unafiki na ufisadi." 

Chanzo cha sakata hili hadi kutua mahakamani ni tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazomkabili Bw. Rostam ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu nchini ambazo baada ya kimya kirefu, alizizungumzia kwa kwa mara ya kwanza alipoalikwa kwenye uzinduzi wa kwaya ya Kanisa la KKT Kinondoni, ambapo mbali na kutoa msaada wa sh. milioni saba, pia alikanusha kuhusika na tuhuma zote hizo na kusisitiza kuwa yeye ni mtu safi mbele ya jamii. 

Siku kadhaa baada ya Rostam kutoa kauli hiyo,Mtikila aliibuka na kulaani kitendo cha Rostam kutoa mchango kanisani na 'kujisafisha' akisema Kanisa halikustahili kupokea fedha za Mbunge huyo. 

Akionekana kukerwa na kitendo hicho, Rostam ndipo alipoitisha mkutano wa Julai 13 ambapo pamoja na kauli iliyoonekana kumuudhi Mtikila alitoa siri kuwa Mchungaji huyo naye aliwahi kumwomba mchango kwa ajili ya kanisa lake na akampa sh. milioni 3. Mtikila hakukana dai ila alihoji uhalali wa risiti ya mchango huo ambayo Rostam aliitoa kwa wanahabari akisema ilighushiwa. 

Katika kesi hiyo, pamoja na kutaka alipwe mamilioni hayo ya fedha Mtikila amembana zaidi Rostam kwa kuiomba Mahakama imwamuru awaombe radhi Watanzania kwa kile Mchungaji huyo alichokisema kuwa ni wazee wa mbunge huyo kujihusisha na biashara ya utumwa. 

Mtikila ameomba katika hati hiyo: "Zaidi (Mahakama) imuamuru mdaiwa wa kwanza (Rostam) aombe radhi kwa maandishi kwa watanzania kwa niaba ya familia yake au mababu zake, kwa kuwafanyia biashara ya utumwa wazee wetu kwa kuwafanyisha kazi za kubeba dhahabu na pembe za ndovu." 

Uchunguzi wa Majira umebaini kuwa dai hilo la Mtikila limetokana na Bw. Rostam kukiri alipozungumza Julai 13 na waandishi wa habari kuwa biashara zake amerithi kwa wazee wake waliokuwa wakifanyabiashara tangu mwaka 1852 ingawa hakutaja aina ya biashara hizo. 

Rostam alisema:"Fedha zangu ni pato halali linalotokana na jasho langu kupitia biashara ambayo imekuwa ikiendeshwa na familia yangu tokea mwaka 1852." 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mwqenendo wa Madai na Kanuni za Mahakama Kuu, Rostam halazimiki kufika mwenyewe mahakamani hapo kujitete, iwapo ataamua kuweka wakili au mtu wa kumwakilisha lakini anaweza kulazimika kufika kortini iwapo kuna ushahidi utakaokuwa muhimu yeye mwenyewe kuutoa.

No comments: