Friday, October 17, 2008

John Meli Aelezea Yaliyomsibu

UNAPOKUTANA na John Meli (55), mara moja utabaini kuwa ni mtu aliyekata tamaa ya kuishi.

Ni kutokana na maisha yanavyomwendea kombo. Ni mlemavu wa mikono yote miwili, ulemavu alioupata ukubwani kiasi cha kumfanya ashindwe kujitegemea kama alivyozoea alipokuwa mtumishi wa Shirika la Reli Tanzania(TRC).

Meli hawezi kukumbuka vizuri hali ilikuwaje hadi akapata ulemavu huo ingawa anajua kuwa mikono yake miwili ilikatwa na mashine.

“Siwezi kusema kwa hakika ni nini kilitokea zaidi ya kuwa nilipostuka, niliona mkono wangu wa kushoto ukiwa tayari umenaswa na mashine na kuvunjika. Nikiwa nimetaharuki nikajikuta natumia mkono wangu wa kulia kuunasua mkono wangu, kumbe ndio nilikuwa najiongezea matatizo makubwa zaidi; mkono wa kulia nao ulikatwa mara moja," anasem Meli.

Alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) tangu mwaka 1975 akiwa katika idara ya ufundi. Alitumikia shirika hilo kwa miaka mitano kabla ya kukumbwa na ajali hiyo kubwa iliyomvurugia ndoto ya maisha yake.

"Nilikuwa nikifanya kazi katika karakana ya kituo kikuu cha reli mkoani Tabora," anakumbuka.

"Huko nilikuwa nikichonga vipuri vilivyohitaajika kwa ajili ya mashine za kupandishia mizigo melini kule Mwanza.

"Siku hiyo wafanyakazi wenzangu walikuwa wamekwenda kula chakula cha mchana. Mimi nilitaka kukamilisha kazi zangu kwanza ndipo niende kuungana nao katika chakula.

"Siwezi kukumbuka vizuri ilitokeaje lakini katika kujaribu kumaliza kazi zangu mapema, nilistukia nimeingiza mkono kwenye mashine na baadaye nikaingiza mkono wa pili na kuupoteza mkono wa kulia, huku mwingine ukiwa umeumia vibaya.

"Sasa naishi kwa kutegemea huruma za watu."

Tukio hilo lilitokea Januari 18, 1980 na baada ya kukatika mikono yote, alikimbizwa hospitali ya Mkoa ya Kitete kwa ajili ya kupata matibabu, lakini tayari "nilikua nimeshaharibikiwa kimaisha".

“Maumivu yalipokuwa yakipungua, nililazimika kuanza kufanya mazoezi ya kuandika kwa kutumia mkono wa kushoto ambao ulipona baadaye. Nilipopata kasi katika kuandika nilibadilishiwa kazi na kuwa karani, kazi ambayo niliifanya kwa ufanisi mkubwa,” anasema mfanyakazi huyo wa zamani wa TRC.

"Hata hivyo, kuna wakati anapata maumivu makali kutoka katika mikono yote miwili, hasa mkono naoandikia na hivyo kuendelea kupata mateso.

“Nadhani pia suala hilo liliingiliana na ile hali ya Ustawi wa Jamii wizara kutoa ufadhili wa mimi kupata mkono wa bandia, kwani kulijenga chuki kutoka kwa baadhi ya watu pale ofisini, wengine wakitaka niwape kitu kidogo.

"Nitawezaje kuwasomesha hawa, hasa Jennifer ambaye yuko kidato cha pili na Ezekiel ambaye yuko kidato cha kwanza," anasema.

“Mahali pa kulala sina shida, na fedha za kujikimu sina. Hivi sasa sasa walau Manispaa ya Dodoma imenisaidia kulipa karo ya wanangu. Wakitoka shule wakati mwingine kunakuwa hakuna chakula, na ninavyoona ni kuwa wanangu wanateseka sana,” anasema Meli.

"Angalau tunaweza kupata Sh1,000 kwa siku, hata kama haikishi mahitaji, inasaidia kukabiliana na tatizo la wakati huo," anasema.

“Nimekata tamaa sana. Natamani hata kujitupa katika gari nife, lakini najua itawaoongezea ugumu wa maisha wanangu.Kwa hakika naomba nisaidiwe mtaji wa kufanya biashara ndogondogo.

"Suala la msingi niwe na fedha iwapo mmoja wa wana familia wangu anaumwa asikose matibabu.”

Akiangalia hali yake, Meli anaona kuwa mashirika na makampuni yao wajibu wa kutathmini sera zao kuhusu watu wanaokutwa na matatizo kama yake.

"Ni vyema kuwa karibu na mtu wa aina hiyo ili kumudu kumsaidia kuendeleza maisha," anasema. "Si vizuri kuwapunguza kazini kwa sababu inakuwa kama ni kuwakomoa.

"Mashirika makubwa kama TRC, Tanesco na mengineyo ni vyema yaige mfano Amboni ambayo mmoja wa wafanyakazi wake alipopata ajali na kukatika mkono, alipangiwa kazi ya kufungua mlango getini alipoonekana ameshindwa kuendelea na majukumu yake ya zamani.

Meli, hata hivyo, hakuondoka kavukavu TRC. Alipata kiinua mgongo kilichomfanya anunue nyumba anayoishi hivi sasa.

Alilipwa Sh16 milioni, ikiwa ni mafao yake yote, lakini akalipwa kifuta jasho cha Sh30,000 mwaka 2003 baada ya kupunguzwa kazi mwaka 1981.

Mzee huyo anayeishi katika eneo la Nkuhungu anawaomba wasamaria wema kumsaidia kupata mtaji wa biashara ndogondogo zitakazoendana na ulemavu alionao, akiamini biashara ya duka dogo linaweza kumsaidia kuendesha maisha yake.


No comments: