Saturday, October 18, 2008

Annan aipokea ripoti juu ya ghasia Kenya

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, na ambaye aliongoza shughuli za upatanishi kufuatia mgogoro wa kisiasa nchini Kenya, ameipokea ripoti ya tume iliyochunguza ghasia nchini humu kufuatia uchaguzi wa rais mwaka jana.

Bw Annan aliipongeza tume hiyo iliyosimamiwa na Jaji Waki, akisema ilitekeleza kazi nzuri.

Alisema ataitisha mkutano kati yake na Rais Mwai Kibaki, na Waziri Mkuu Raila Odinga, ili kushauriana juu ya hatua zitakazofaa.

Uchunguzi wa tume hiyo utaendelewa kuhifadhiwa kwa siri, hadi pale hatua muwafaka zitahitajika kuchukuliwa.

Bw Annan alielezea kwamba anafahamu kuna hisia miongoni mwa wengi kutaka kujua ni nani aliyetajwa, au hakutajwa katika uchunguzi wa tume hiyo, lakini alisema ni vyema kuepuka kuwaza hayo, hadi pale kiongozi wa mashtaka, au jaji atakapofungua kesi na kuanza kazi yake.

Alielezea kwamba ni muhimu kufuatia utaratibu unaofaa, hasa katika kuheshimu haki za mtu binafsi, na hii sio mara ya kwanza kuzingatia utaratibu kama huo.

Alisema anaamini ikiwa wote wataheshimu na kuzingatia utaratibu huo, basi utekelezaji utawezekana.

No comments: