Wednesday, October 29, 2008

Wahariri Waandamana Dar

WAHARIRI na wadau wengine wa habari nchini, jana waliandamana kutoka mtaa wa Lugoda mpaka Ofisi ya Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, huku wakiwa wameziba midomo yao kwa plasta. 

Wadau hao walikuwa wakipinga hatua ya Serikali kufungia gazeti la MwanaHALISI huku wakisema bila uhuru wa vyombo vya habari nchini, kashfa za ufisadi kama za Richmond na EPA zingeendelea kulitafuna Taifa. 

Gazeti la MwanaHALISI lilifungiwa na Serikali kwa miezi mitatu, kutokana na kile kilichoelezwa kuandika habari za uchochezi kuhusu njama za baadhi ya viongozi wa CCM kujipanga kumng'oa Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2010. 

Wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali kupinga hatua hizo, wadau hao waliweka historia nchini kwa wanahabari kuandamana kupinga hatua za kuingiliwa uhuru wa vyombo vya habari. 

Baada ya kufika kwenye ofisi za Wizara hiyo, waraka maalumu uliokuwa na ujumbe wa maandamano hayo, ulipokewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Habibu Nyundo na kuahidi kuufikisha kwa Waziri husika ambaye kwa sasa yuko bungeni Dodoma. 

Hata hivyo, katika hotuba yake, Bw. Nyundo alidai kuwa Jukwaa la Wahariri halitambuliki kisheria, kwani tayari jina hilo lilishawahi kusajiliwa awali na wahariri wa zamani na aliwataka kubadilisha na kujisajili upya ili watambulike. 

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Bw. Absalom Kibanda, alisema kitendo cha Serikali kuchukua hatua ya kufungia magazeti ni dalili za wazi za kuishiwa uvumilivu na pengine kuwa mwanzo wa dhamira inayolenga kuendelea kuvibana vyombo huru vya habari, kwa kutumia sheria za zamani kuvikandamiza. 

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-Tan), Bw. Ayoub Rioba, alisema hii ni nchi yenye mfumo wa kidemokrasia na inayofuata mfumo wa soko huria, hivyo Serikali haina budi kulinda na kusimamia vyema vyombo vya habari na si kuvikandamiza kwa maslahi ya watu wachache. 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bibi Ananilea Nkya, alieleza kukerwa na hatua za kufungiwa MwanaHALISI. 

"Ni jambo la hatari kufungia vyombo vya habari kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwaziba midomo wananchi ili wasitoe hisia zao kwa manufaa ya Taifa zima," alisema. 

Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiliunga mkono maandamano hayo katika ilichokiita salamu zake za mshikamano kwa wanahabari nchini zilizotolewa jana na Mkurugenzi wa Vijana wa Chama hicho, Bw. John Mnyika. 

"Tunawapongeza wahariri kwa mshikamano wenu katika kipindi hiki cha majaribu; endeleeni kusimama pamoja, ni umoja wenu ndio utakaokuwa kinga ya pamoja dhidi ya mtu au chombo chochote kinachoingilia uhuru wenu. 

"Mshikamano wenu ni ishara ya kushindwa kwa mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ na imani kwamba umoja ni nguvu. Wahariri wote hawapaswi kukaa kimya kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI, kwa kuwa leo ni kwa gazeti hilo, kesho itakuwa kwa gazeti lingine; hivyo ni vyema kuungana kulinda uhuru, taaluma na sekta ya habari," alisema. 

Chama hicho kililaumu jinsi hatua hizo zilivyochukuliwa kwa kusema ni sawa na Serikali kuamua kesi ambayo yenyewe ndiyo ilikuwa imelalamika. 

"Hatua ya Waziri mwenye dhamana na sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashitaka na mfungaji ni mwelekeo mbovu wa kupuuza taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki. 
"Uamuzi uliofanywa na Serikali hauna tofauti na unaofanywa na raia wanaojichukulia sheria mikononi(mob justice). 

"Kwa Serikali inayoheshimu misingi ya asili ya haki, tulitarajia chombo chochote cha habari, kikivunja sheria ama kukiuka maadili dhidi ya serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashitaka au malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la Habari (MCT) au Mahakama," aliongeza. 

Wakati huo huo, mwandishi wetu Hilary Komba, anaripoti kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Oganaizesheni, Kampeni na Uchaguzi ya NCCR-Mageuzi, Bw. Faustin Sungura, alisema wahariri hawakupaswa kuandamana bila kwanza kujiridhisha iwapo habari iliyosababisha gazeti kufungiwa ilifuata maadili ya kitaaluma na kwamba ilikuwa ya kweli. 

"Maandamano ya wahariri hayakutakiwa kufanyika kabla ya kufanyika uchunguzi wa kina, kwa sababu kwa sasa kuna baadhi ya watu wamejitokeza wanataka kulishitaki gazeti hilo sasa kama litaonekana lina hatia mahakamani basi wahariri watajiweka katika nafasi mbaya," alisema Bw Sungura. 

Kwa maoni yake, alisema wahariri wameharakisha kuandamana kabla hata ya kufanya uchunguzi kwani inaweza kuwashushia hadhi yao, ambayo ni muhimu katika Taifa ambalo linawahitaji kwa kazi zao. 

Alisema wahariri wana haki ya kuandamana kama haki zao zikiwa zimekiukwa kama kufungiwa magazeti, lakini wanapaswa kufahamu kuwa jambo wanalodai lazima liwe limefanyiwa kazi kwanza. 

Aliongeza kuwa iwapo ingebainishwa kwanza ukweli wa habari hiyo, hata chama chake kingekuwa tayari kushirikiana kwa karibu zaidi kupinga hatua iliyochukuliwa ya kulifungia gazeti la MwanaHALISI.

No comments: